Takribani wananchi 14,420 wa Shehia za Vijibweni ,Mbiji,Karange,Mtambile na Njia ya Mtoni Kisiwani Zanzibar wamepunguziwa adha ya kufuata huduma ya vipimo vya afya mbali na eneo lao baada ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kugharamia ununuzi wa kifaa tiba kilichokosekana tangu kuanza kwa kituo hicho .

Akikabidhi Kifaa hicho kwa uongozi wa kituo cha Afya cha Donge Vijibweni, Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ Mhe. Mihayo Juma Nung’a amepongeza hatua hiyo ya TASAF ambayo amesema inatekeleza kwa vitendo lengo la serikali la kuwaondolea wananchi kero ya upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwemo ile ya afya

“ninawaagiza kutunza mashine hii ili wananchi waweze kunufaika kwa muda mrefu na kusahau madhira waliyokumbana nayo kabla ya kupata mashine hiyo” alisisitiza Mhe.Mihayo.

Aidha Naibu Waziri huyo amezungumzia umuhimu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na TASAF kuwa ni mkombozi kwa wananchi waliokuwa wanaishi katika umaskini mkubwa na hivyo kuzitaka kaya husika kutumia ruzuku inayotolewa kwa uangalifu huku akitilia mkazo suala la uanzishaji wa miradi ya kiuchumi ili kujiongezea kipato.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ambaye pia alihudhuria hafla ya kukabidhi mashine hiyo amesema taasisi yake itaendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha maisha ya wananchi katika sekta mbalimbali ikiwemo ile ya afya.

Amesema kwa kutambua umuhimu wa uboreshaji wa afya za wananchi, TASAF imeweka kipengele cha afya kuwa moja ya masharti katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambapo watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wanapaswa kuhudhuria kliniki kila mwezi.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kituo hicho Miza Ali Ussi amesema kituo kilikuwa na ukosefu mkubwa wa mashine hiyo na hivyo kuwalazimu wananchi kufuata huduma hiyo katika maeneo yaliyoko mbali na eneo hili jambo lililokuwa linawatatiza kwa kiwango kikubwa.

pic1

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe.Mihayo Juma Nung’a (aliyevaa shati la drafti) akimkabidhi mashine ya kupimia damu afisa tabibu Miza Ali Ussi wa kituo cha afya cha Donge Vijibweni kisiwani Zanzibar.Kifaa hicho kimenunuliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF-.Kushoto nio Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,bw. Ladislaus Mwamanga.

pic2

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bwana Ladislaus Mwamanga,(aliyesimama) akizungumza katika hafla ya kukabidhi mashine ya kupimia maradhi kilichonunuliwa na TASAF kwa ajili ya kituo cha Donge Vijibweni kisiwani Zanzibar.Kushoto kwake ni Naibu Waziri katika ofisi ya makamu wa pili wa Rais wa SMZ,Mhe. Mihayo Juma Nung’a.

pic3

Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa SMZ,Mhe. Mihayo Juma Nung’a  (hayupo pichani) katika hafla ya kukabidhi mashine ya kupimia maradhi iliyonunuliwa na TASAF kwa ajili ya kituo cha Afya cha Donge Vijibweni huko Zanzibar.

pic4

pic5

Sehemu ya jengo la kituo cha Afya kinachohudumia takribani wananchi 14,420 kilichojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF katika eneo la Donge Vijibweni kisiwani Zanzibar.

 

Add comment


Security code
Refresh