Featured Interventions

Ujumbe wa Maafisa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo-DRC- umewasili nchini kwa ziara ya siku 10 kujifunza namna Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Maendeleo ya jamii –TASAF ilivyofanikiwa kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini-PSSN.

Akiwakaribisha Maafisa hao kwenye Ofisi ndogo za TASAF jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko huo Bwana Ladislaus Mwamanga amebainisha hatua mbalimbali zilizochangia kufanikiwa kwa Mpango huo wa Kunusuru Kaya Maskini unaohudumia Zaidi ya Kaya Milioni MOJA NA LAKI MOJA nchini kote.

Bwana Mwamanga amesema mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo yametokana na ushirikishwaji wa jamii huku akisema mchango wa Serikali ya Tanzania na Wadau mbalimbali za Maendeleo umechangia kwa kiwango kikubwa kufanikisha Mpango huo wa aina yake kupata kutekelezwa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TASAF amewaambia Maafisa hao kutoka DRC kuwa Mfuko huo tangu kuanzishwa kwake umejikita zaidi katika kuboresha huduma za kijamii hususani katika sekta za elimu, afya,maji,mazingira,na kuhamasisha walengwa kuanzisha shughuli za uzalishaji mali ili waweze kukuza uchumi na kupunguza umaskini.

Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe huo bwana Ruphin Kimuemue Bo- Elongo amesema lengo la ziara hiyo ni kujifunza namna serikali ya Tanzania kupitia TASAF ilivyofanikiwa kuwahudumia wananchi hususani wanaoishi katika hali ya umaskini .

Amesema wamevutiwa na mafanikio ambayo TASAF imeyapata katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao wamesema utaisaidia pia DRC kutokana na kuwa na wananchi wake wengi wanaishi katika adha ya umaskini.

Ukiwa katika ofisi za TASAF ujumbe huo umepata fursa ya kufahamishwa utekelezwaji wa shughuli za taasisi hiyo zikiwemo za Ajira za Muda ,Uhawilishaji Fedha, na Uwekaji wa Akiba kwa Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

Maafisa hao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo pia watatembelea wilaya ya Kibaha mkoani Pwani ,Temeke na Zanzibar ambako watakutana na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kujionea namna wanavyonufaika na huduma za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF.

 pic1

Ujumbe kutoka DRC ukimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,(anayeitazama kamera) kwenye ukumbi wa ofisi ndogo ya TASAF jijini DSM.

pic2

pic3

Mkurgenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga (wa tatu kulia ) akiwa katika picha ya pamoja na ujumbe kutoka DRC ambao uko nchini kujifunza shughuli za huduma ya hifadhi ya jamii