TASAF YAOKOA WATOTO KATIKA KAZI ZA UCHIMBAJI WA MADINI MKOANI KATAVI

User Rating: 2 / 5

Star ActiveStar ActiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Tatizo lililokuwa linaukabili mkoa wa Katavi la watoto kutoka katika kaya maskini kuacha masomo na kutafuta vibarua kwenye migodi ya machimbo ya madini,limepungua kwa kiwango kikubwa baada ya kuanza kutekelezwa kwa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF.

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda Bibi. Lilian Charles Matinga amesema hayo mwishoni mwa wiki alipofungua Warsha ya Wandishi wa Habari wa mkoa wa Katavi juu ya Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini .

Bi.Matinga amesema kupungua kwa tatizo la ajira ya Watoto kumetokana na moja ya masharti ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini  unaohimiza watoto kuhudhuria masomo kwa zaidi ya asilimia 80 kwa mwezi ili waweze kupata huduma za Mpango.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya amesema walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, wameanza kuboresha maisha kwa kujenga nyumba za kudumu huku wengine wakijiongezea kipato kwa kuanzisha biashara ndogo ndogo kama ufugaji wa kuku,bata, nguruwe na wengine kukuza shughuli za kilimo.

Ili miradi ya Walengwa hao wa TASAF iweze kupata mafanikio yanayotarajiwa ,Mkuu huyo wa Wilaya ameagiza Wataalam wa ugani kuweka mipango ya kuwatembelea walengwa na kuona namna ya kuwasaidia kuboresha miradi wanayoianzisha.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Mtaalamu wa Mawasiliano wa TASAF,Bi. Zuhura Mdungi amesema baada ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kufikia takribani miaka minne sasa , katika maeneo mengi ya utekelezaji wa Mpango ,walengwa wameboresha maisha yao huku kukuwa na mafanikio makubwa katika nyanja za elimu, afya na uanzishaji wa miradi midogo midogo ya kiuchumi.

Zifuatazo ni picha za ufunguzi wa Warsha hiyo.

pic1

Mkuu wa wilaya ya Mpanda ,Bi.Lilian  Charles Matinga (aliyesimama) akisoma hotuba ya ufunguzi wa warsha ya waandishi wa habari juu ya Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Katavi. Kulia kwake na Mtaalamu wa Mawasiliano wa TASAF,Bi. Zuhurua Mdungi na kushoto kwake ni Mratibu wa TASAF wa mkoa wa Katavi .

pic2

Mtaalamu wa Mawasiliano wa TASAF,Bi. Zuhura Mdungi (aliyesimama) akitoa mada kwenye warsha ya waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na TASAF mkoani Katavi.

pic3

Baadhi ya Waandishi wa Habari wa mkoa wa Katavi wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Mpanda Bi. Lilian Charles Matinga (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa warsha juu ya kuwajengea uelewa wa Shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini. 

pic4

Moja ya nyumba zilizojengwa na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini kwa kutumia ruzuku wanayopata kutoka TASAF katika halmashauri ya wilaya ya Mpanda mkoani Katavi.

KAMATI YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU YAVUTIWA NA UTENDAJI KAZI WA TASAF

User Rating: 3 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar InactiveStar Inactive

Halmashauri ya wilaya ya Kibaha mkoani Pwani ni miongoni mwa maeneo yanayotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF. Miradi inayotekelezwa kupitia mpango huu ni pamoja na uhawilishaji fedha kwa kaya maskini, kutoa ajira ya muda kwa walengwa, kuweka akiba na kukuza uchumi wa kaya na ujenzi wa miradi ya miundo mbinu.

Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, wametembelea kijiji cha vikuge, kilichoko katika halmashauri ya Kibaha, mkoa wa Pwani kwa lengo la kubadilishana uzoefu wa namna Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unavyotekelezwa.

Walengwa wa TASAF wa kijiji cha Vikuge wameanzisha miradi mbalimbali ya kujiongezea kipato na kujikwamua na umaskini. Miongoni mwa miradi inayotekelezwa na Walengwa hao ni ufugaji wa kuku,bata,ususi wa vikapo na mikeka na uuzaji wa bidhaa zikiwemo sabuni,nazi, nguo.

 pic1

Bidhaa zinazopatikana, katika kijiji cha Vikuge

Wajumbe wa kamati hiyo walipata fursa ya kujifunza namna mpango wa kuweka na kukuza uchumi kwa kaya unavyotekelezwa. Mradi huu unalenga kuwajengea walengwa uwezo wa kuweka akiba kidogo kidogo katika vikundi na kukopeshana kwa lengo la kuanzisha miradi midogo midogo ya kiuchumi.

Kupitia mpango wa kukuza uchumi wa kaya, wana Vikuge wamefanikiwa kuunda vikundi vyenye jumla ya Walengwa 15 kwa kikundi. Ambapo kamati iliweza kuonana na kukundi kimojawapo kiitwacho Twabaha ambacho kimeweza kujiwekea akiba ya shilingi 600,000 kwa kipindi cha miaka miwili. Wana Twabaha hugawana hisa kila baada ya mwaka mmoja na kuwekeza faida wanayopata kutokana shughuli za kikundi.

 pic2 

Mradi mwingine uliovutia wajumbe wa kamati ya kusimamia viongozi wakuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni ule wa shamba darasa. Mradi huu unatakelezwa kupitia mpango wa kukuza uchumi wa kaya, umeanzishwa ili kuwakutanisha walengwa na maafisa ugani ambao hutoa mafunzo ya namna ya kuboresha shughuli za kilimo ili kuongeza tija.

Kupitia utaratibu huo Mlengwa hufanya kazi kwa karibu na mtaalam wa kilimo kwa hatua zote muhimu wa utayarishaji wa shamba hadi mavuno.Swa Vikuge. Shamba darasa hilo limepandwa mihogo, na walengwa hupata fursa ya kujifunza kilimo bora na cha kibiashara .

 pic3

Wajumbe wa Kamati wakifuatilia maelezo toka kwa afisa ugani.

 

 Wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais mhe.Mihayo Musa Nunga waliipongeza TASAF kwa kubuni mikakati mbalimbali ya kusaidia jitihada za serikali za kuwakwamua wananchi kutoka katika dimbwi la umaskini na kutoa wito kwa walengwa kutumia fursa hiyo vizuri ili waweze kunufaika nayo.

WAZIRI MKUCHIKA AVUTIWA NA MIRADI YA TASAF

User Rating: 5 / 5

Star ActiveStar ActiveStar ActiveStar ActiveStar Active

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mhe. George Mkuchika amepongeza hatua ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kubuni utaratibu mzuri wa kuwashirikisha wananchi katika ujenzi wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

Mhe. Mkuchika amesema utaratibu huo siyo tu kwamba unapunguza gharama bali unawafanya wananchi kuithamini miradi hiyo na kuitunza kutokana na kutumia nguvu na jasho lao katika kuitekeleza.

Waziri huyo ameyasema hayo mwishoni mwa juma baada ya kutembelea kijiji cha Mwahango katika halmashauri ya wilaya ya Singida ambako alikagua jengo la zahanati lililojengwa na TASAF kwa kuwashirikisha wananchi kijijini hapo.

Aidha Mhe. Mkuchika ameupongeza mkoa wa Singida kwa kusimamia zoezi la uandikishaji Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwa uaminifu na hivyo kupunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya Watu wasiostahili kujumuishwa kwenye Mpango huo kinyume cha utaratibu.

Akiwa kijijini hapo Waziri Mkuchika alipata ushuhuda wa mafanikio waliyoyapata baadhi ya Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya masikini ambao wameweza kuboresha maisha yao katika nyanja za makazi, lishe,uanzishaji wa miradi ya kiuchumi ,kusomesha watoto na kujiunga na mfuko wa bima ya afya ya jamii na hivyo kupata huduma ya matibabu katika kipindi chote cha mwaka.

Taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TASAF mkoani Singida imeonyesha kuwa, mafanikio makubwa yamepatikana tangu kuanza utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya maskini mkoani humo hususani katika kuamsha ari ya wananchi kuuchukia umaskini kwa vitendo.

Hata hivyo taarifa hiyo imeiomba serikali kupitia TASAF kukamilisha zoezi la kuvijumuisha vijiji vingine ambavyo wananchi wao hawakupata fursa ya kunufaika na huduma za Mpango katika awamu ya kwanza ya utambuzi iliyofanyika mkoani humo mwaka 2014.

Waziri Mkuchika amesema serikali inalifanyia kazi suala hilo kwa juhudi zaidi kwani utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya maskini umefanyika kwa asilimia 70 tu kutokana na ufinyu wa fedha ,hata hivyo kutokana na Mpango huo kuwagusa wananchi wanaokabiliwa na umaskini moja kwa moja, utaratibu mzuri unaaandaliwa ili wananchi wote wanaostahili kujumuishwa kwenye Mpango waweze kutambuliwa hususani katika vijiji ambavyo havinufaiki na Mpango huo kwa sasa.

Zifuatazo ni picha za tukio hilo. 

 pic1

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika akikagua jengo la zahanati ya kijiji cha Mwahango katika wilaya ya Singida jengo lililojengwa na TASAF ikiwa ni mkakati wa kuwasogezea huduma ya Afya wananchi na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

pic2

Waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika akitoka katika jengo la zahanati ya kijiji cha Mwahango katika halmashauri ya wilaya ya Singida lililojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo.

pic3

Mwonekano wa jengo la zahanati ya kijiji cha Mwahango katika halmashauri ya wilaya ya Singida iliyojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF kwa kushirikiana na wananchi wa eneo hilo ikiwa ni mkakati wa TASAF wa kuboresha huduma za Afya kwa walengwa wake na wananchi  wa eneo hilo.

pic4

Waziri Mkuchika akipanda mche wa mti katika eneo la Zahanati ya kijiji cha Mwahango katika halmashauri ya wilaya ya Singida iliyojengwa na TASAF na wananchi.

pic5

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika (aliyesimama mbele ya kamera) akiwahutubia baadhi ya watumishi wa sekretarieti ya mkoa wa Singida wakati alipofanya ziara ya kikazi mkoani humo.