MKUTANO KAZI BAINA YA WADAU WA MAENDELEO, MAAFISA WA SERIKALI NA WATENDAJI WA TASAF WAMALIZIKA KWA MAFANIKIO JIJINI DAR ES SALAAM

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Mkutano wa Wadau wa Maendeleo ,Maafisa wa Serikali na Watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF uliojadili kwa kina utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao unatekelezwa na Serikali kupitia TASAF umemalizika jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo ambao hufanyika kila baada ya miezi sita , umefanyika kufuatia ziara ya washiriki hao katika wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza na Unguja ambako walikutana na Walengwa wa Mpango huo na kujionea namna Walengwa wanavyoendelea kunufaika na huduma zinazotolewa na Mpango huo kuboresha maisha yao.

Miongoni mwa mambo yaliyofanywa katika mkutano huo ni pamoja na kuweka mkakati wa utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpangowa Kunusuru Kaya Maskini inayotarajiwa kuanza Mwezi Aprili hapo mwakani ambayo italenga zaidi katika kuwashirikisha Walengwa kufanyakazi za maendeleo kwenye maeneo yao na kisha kulipwa ujira.

Akizungumza na Washiriki wa Mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga ametoa wito maalumu kwa wadau na maafisa wa Mfuko huo kufanya kazi kwa bidii na kuweka mbele maslahi ya taifa ili lengo la serikali la kuwapunguzia kero ya umaskini wananchi liweze kufikiwa kwa ufanisi.

Bwana Mwamanga amesema utekelezaji na mafanikio ya Mpango huo unategemea kwa kiwango kikubwa jitihada za pamoja hasa ikizingatiwa kuwa wananchi wanaolengwa ni wale ambao kwa kiwango kikubwa wamekuwa wakiishi katika hali ya umaskinina wengine kukata tamaa jambo ambalo amesema linapaswa kukabiliwa kwa nguvu za pamoja.

Kwa upande wake Kiongozi wa shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia hapa nchini Bwana Mohamed Muderis amepongezea jitihada za dhati zinazofanywa na Watumishi wa TASAF na wadau wengine katika kuwahudumia Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na hivyo kuleta hamasa ya dhati ya Walengwa kuuchukia umaskini.

Aidha Bwana Muderis ametoa rai kwa watumishi hao kuendelea na kukamilisha kwa wakati maandalizi ya sehemu ya pili ya Mpango wa kunusuru kaya maskini inayotarajiwa kuanza mapema mwakani na kuzingatia kwa dhati maelekezo ya serikali.

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF upo kwenye maandalizi ya sehemu ya pili ya Mpango wa kunusuru Kaya Maskini baada ya kukamilika kwa sehemu ya kwanza huku mkazo ukiwekwa kuwawezesha walengwa kushiriki katika kazi za Ajira ya Muda, kuunda vikundi vya kuweka akiba na kukopeshana,ujenzi wa miundombinu hasa katika sekta za elimu, afya ,maji na kuanzisha shughuli za uzalishaji mali ili kujiongezea kipato.

 pic1

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladslaus Mwamanga (katikati) akiongoza mkutano wa Wadau wa Maendeleo, Maafisa wa Serikali na TASAF kwenye ukumbi wa Mfuko huo jijini Dar es Salaam.

 pic2

Picha ya juu na chini menejimenti ya TASAF na ile ya Benki ya Dunia hapa nchini wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa TASAF, Serikali Na Wadau wa Maendeleo baada kuhudhuria mkutano wao wa pamoja jijini Dar es Salaam.

pic3

pic4

Mmoja wa Watumishi wa TASAF,Shadrack Mziray akiwasilisha taarifa kwenye Mkutano wa Wadau ,serikali na TASAF jijini Dar es salaam.

pic5

Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Wadau ,Serikali na TASAF wakiwa kwenye ukumbi wa Mikutano wa TASAF jijini DSM katika mkutano uliojadili utekelezaji wa Shughuli za Mfuko huo na maandalizi ya awamu ya pili ya Mpango huo inayotarajiwa kuanza hapo mwakani.

WADAU WA MAENDELEO WAKUTANA NA MENEJIMENTI YA TASAF

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Wadau wa Maendeleo na menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF- wamekutana jijini DSM kwenye Ofisi Ndogo za Mfuko huo Kujadili pamoja na mambo mengine maandalizi ya zoezi la kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini litakalofanyika mwanzoni mwa mwezi ujao.

Utaratibu huo wa kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini hufanyika mara mbili kwa mwaka na hujumuisha Maafisa wa Serikali  na wadau wa Maendeleo wa ndani na nje ya nchi ambao hupata fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo na kukutana na Walengwa na Viongozi wa Maeneo ya Utekelezaji wa Mpango.

Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF imekuwa ikitekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini –PSSN- ulioanza mwaka 2012 katika baadhi ya Halmashauri za Wilaya kwa majaribio na kisha kutekelezwa nchini kote kufuatia mafanikio ya majaribio yaliyofanyika katika wilaya za Bagamoyo, Kibaha, Chamwino na Mbarali mkoani Mbeya.

Kwa sasa Mpango huo unanufaisha Kaya takribani Milioni Moja na Laki Moja Tanzania Bara ,Unguja na Pemba ambako walengwa hupata ruzuku ya Masharti hususani katika nyanja za elimu na afya na ile isiyokuwa ya Masharti kwa lengo la kuboresha maisha ya walengwa .

Kufuatia utekelezaji wa Mpango huo wa Kunusuru Kaya Maskini, Walengwa wa Mpango huo wameonyesha mabadiliko makubwa hususani katika uboresha ya makazi ,uanzishaji wa miradi ya kiuchumi  huku suala la mahudhurio ya wanafunzi wanaotoka kwenye Kaya hizo shuleni na kwenye vituo vya afya yakiboreshwa zaidi.

Serikali kupitia TASAF kwa sasa iko katika maandalizi ya Awamu ya Pili ya utekelezaji wa Mpango huo ambayo mkazo maalum utawekwa kwa Walengwa kufanya kazi na kuibua miradi itakayowaondolea kero kwa kushirikiana na Wataalamu walioko kwenye maeneo yao huku pia mkazo mkubwa ukiwekwa kwenye shughuli za uzalishaji mali ili waweze kukuza uchumi wao na hivyo kupunguza umaskini.

 pic1

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw.Ladislaus Mwamanga (katikati) akimsikiliza kiongozi wa Shughuli za TASAF katika Benki ya Dunia Bw. Mohamed Muderis (mwenye miwani)

pic2

Wadau wa Maendeleo na Menejimenti ya TASAF (picha ya juu na chini wakiwa katika mkutano wa kujadili utekelezaji wa Shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini jijini DSM.

pic3

pic4

pic5

Menejimenti ya TASAF wakiwa katika mkutano na Wadau wa Maendeleo kwenye ukumbi wa Mikutano wa Mfuko huo kujadili masuala ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko huo jijini DSM.

MAKAMU WA RAIS WA BENKI YA DUNIA KANDA YA AFRIKA, DR. HAFEZ GHANEM AVUTIWA NA MAFANIKIO YA SERIKALI KATIKA KUPAMBANA NA UMASKINI KUPITIA TASAF.

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika,Dr. Hafez Ghanem amefanya ziara katika mtaa wa Mamboleo,halmashauri ya wilaya ya Temeke jijini DSM na kukutana na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF.

Akizungumza na Walengwa hao baada ya kukagua bidhaa wanazozitengeneza kama njia mojawapo ya kukuza kipato chao, Dr. Ghanem amesema jitihada waliyonyesha Walengwa hao ya kuuchukia Umaskini ,itaendelea kuungawa mkono na Benki hiyo ya Dunia ambayo amesema ni rafiki mkubwa wa Serikali ya Tanzania.

Dr.Ghanem ametoa rai maalum kwa Walengwa hao wa TASAF kutumia fursa hiyo kuongeza uzalishaji mali na kutumia mazingira mazuri ya kujiletea maendeleo kwani amesema ni dhahiri kuwa serikali ya Tanzania inawajali na imeonyesha utayari wa kuboresha maisha ya wananchi.

Aidha Makamu huyo wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika ambaye aliambatana na Mkurugenzi Mkazi wa  Benki hiyo Bi. Bella Bird, amesisitiza kuwa taasisi hiyo kubwa ya fedha Duniani itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kufadhili Mpango huo wa Kunusuru Kaya Maskini kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha utekelezaji wake.

Akizungumza kwenye Mkutano huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bw. Ladislaus Mwamanga ameelezea mafanikio makubwa ambayo Mfuko huo umepata tangu kuanzishwa kwake takribani miaka 18 iliyopita hususani katika nyanja za elimu,afya,maji, na uchumi.

Bw. Mwamanga amesema mafanikio makubwa yaliyopatikana yametokana pia na usimamizi wa Karibu wa viongozi wa Serikali katika ngazi zote za utekelezaji ambapo wamekuwa wakiwahamasisha wananchi kutumia vizuri fursa hiyo ili waweze kuinua kiwango chao cha maisha na kutokomeza umaskini kwa kasi kubwa zaidi.

Benki ya Dunia pamoja na taasisi nyingine za Kimataifa imekuwa ikichangia fedha kugharamia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao kwa sasa unahudumia takribani kaya Milioni Moja na Laki Moja Tanzania Bara, Unguja na Pemba,Mpango ambao umekuwa chachu ya maendeleo kwa Kaya za Walengwa.

 pic1

Makamu Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika,Dr.Hafez Ghanem,akivishwa skafu alipowasili kwenye mtaa wa Mamboleo,wilayani Temeke jijini DSMalipokutana na Walengwa wa TASAF.

pic2

Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Kanda ya Afrika, Dr. Hafez Ghanem akiwa katika picha ya pamoja na  baadhi ya wanafunzi ambao wazazi wao wako katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa na serikali kupitia TASAF.

pic3

Baadhi ya walengwa wa TASAF wa Mtaa wa Mamboleo-Temeke jijini DSM wakiwa katika picha ya pamoja na Makamu wa Rais wa WB kanda ya Afrika Dr. Hafez Ghanem na viongozi wengine akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Ladislaus Mwamanga kulia kwa Makamu huyo wa Rais wa WB.

pic4

pic5