WALENGWA WA TASAF MKOANI KILIMANJARO WAIANGUKIA SERIKALI.

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Mkuchika yuko katika ziara ya kikazi mkoani Kilimanjaro kukutana na wananchi wanaonufaika na huduma za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF kupitia Mpango wake wa Kunusuru Kaya Maskini- PSSN.

Akiwa katika ziara hiyo, Mhe. Mkuchika amejionea namna Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, walivyoboresha maisha yao kwa kutumia huduma za TASAF kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini zinazoambatana na ruzuku ya fedha, elimu ya ujasiliamali na utekelezaji wa masharti ya Elimu na Afya huku mkazo ukiwekwa katika kuwajengea mazingira ya kukuza kipato cha Walengwa hao.

Akizungumza na Walengwa katika wilaya za Same, Mwanga,Siha na Hai kwa nyakati tofauti ,Mhe. Mkuchika amesema shughuli za TASAF ni mwendelezo wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya 2015 ambayo imeielekeza serikali kutumia mbinu mbalimbali za kutatua kero ya umaskini miongoni mwa wananchi kwa lengo la kuboresha maisha yao.

Amesema kutokana na dhamira thabiti ya serikali katika mapambano dhidi ya Umaskini , wananchi kwa ujumla wao hususani wale waliojumuishwa kwenye Mpango wa TASAF wanapaswa kujituma zaidi katika kuanzisha na kutekeleza miradi ya uzalishaji mali ili waweze kujiongezea kipato na hatimaye kuondokana na adha ya umaskini.

Waziri huyo wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amesema kwa kiwango kikubwa amevutiwa na jitihada zilizoonyeshwa na sehemu kubwa ya Walengwa wa TASAF kwa kutumia vizuri huduma za Mfuko huo ambazo amesema zimeanza kuboresha maisha yao na kuamusha ari ya kujiletea maendeleo kwa kufanya kazi kwa bidi zaidi.

Amesema uboreshaji wa makazi ,ufugaji wa mbuzi,kuku,bata na hata ng’ombe unaofanywa na Walengwa hao wa TASAF ni kieleleza tosha cha namna wananchi hususani waliokuwa wakiishi katika umaskini, walivyo na ari kubwa ya kujiondoa kwenye umaskini wa kipato jambo ambalo amesema serikali itaendelea kuwaunga mkono kwa kuwawekea mazingira wezeshi ya kufanikisha azma yao hiyo.

Aidha amesema hivi sasa mipango ya kujumuisha vijiji ambavyo havikupata fursa ya Mpango huo wa TASAFiko mbioni na kuwa wananchi ambao katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Mpango wa kunusuru kaya maskini hawakujumuishwa , watapata fursa hiyo katika awamu ijao ya utekelezaji wake baada ya wananchi wengi kuendelea kuomba huduma hizo za TASAF.

Kwa upande wao baadhi ya Walengwa licha ya kuipongeza Serikali kupitia TASAF ,wameomba huduma za Mfuko huo ziendelee kuwasaidia wao na Wananchi wengine ambao kwa sasa wanaishi katika umaskini mkubwa lakini hawakupata fursa ya kutambuliwa na kuandikishwa kwa utaratibu wa Mfuko huo.

“Baadhi ya wenzetu kwenye vijiji vyetu hawanufaiki na utaratibu huu mzuri wa serikali kupitia TASAF lakini nao pia wanakabiliwa na umaskini ,tungeliomba serikali kupitia TASAF iwafikirie pia” amesema bi. Upendo Issa mkazi wa kijiji cha Kileo,wilaya ya Same.

Zifuatazo ni baadhi ya picha za ziara hiyo ya Mhe. Mkuchika.

pic1

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika (aliyevaa kofia) akikagua nyumba inayojengwa na mmoja wa Walengwa wa TASAF (wa kwanza kulia ) katika kijiji cha Kileo,wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.

pic2

Waziri wan chi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Mkuchika (katikati waliosimama) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya walengwa wa TASAF katika wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro baada ya kuzungumza nao juu ya manufaa wanayoyapata kutokana na huduma za mfuko huo.

pic3

Mhe. George Mkuchika Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (aliyevaa koti nyeusi ) akihesabu fedha kabla ya kumkabidhi mmoja wa Walengwa wa TASAF mkoani Kilimanjaro baadhi ya kuridhishwa na jitihada za mlengwa huyo katika kupambana na umaskini kwa kutumia ruzuku ya TASAF.

pic4

Waziri Mkuchika akiangalia moja ya mazizi ya mbuzi za Walengwa wa TASAF katika wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro ikiwa ni mojawapo ya njia za kujiongezea kipato kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

pic5

Kaimu Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Mhe. Kippi Warioba(wa pli kulia )akieleza jambo baada ya Waziri wa nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora mhe. George Mkuchika kutembelea mojawapo ya makazi ya Mlengwa wa TASAF (mwenye kilemba) wilayani Siha. 

TASAF YAIVUTIA NIGERIA NA SUDAN KUSINI,WAJA NCHINI KUJIFUNZA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA KUNUSURU KAYA MASKINI.

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF yameanza kuvutia Mataifa mbalimbali ya kiafrika kuja nchini kujifunza namna Mpango huo unavyotekelezwa.

Miongoni mwa nchi ambazo zimetuma wataalamu kujifunza namna serikali ya Tanzania kupitia TASAF inavyotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaohudumia takribani kaya Milioni Moja na Laki Moja ni pamoja na Sudan Kusini na Nigeria.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti viongozi wa Ujumbe huo ambao umeanza ziara katika Ofisi za TASAF jijini Dar es salaam,wamepongeza hatua ya Serikali ya Tanzania kutekeleza Mpango huo ambao wamesema unawagusa moja kwa moja wananchi wanaokabiliwa na umaskini.

Wamesema mkakati huo wa kupunguza umaskini kwa njia ya hifadhi ya jamii unaonyesha mafanikio makubwa nchini Tanzania na hivyo kuvutia nchi nyingine kuja kujifunza namna Mpango huo uliyofanikiwa.

Aidha wajumbe hao kutoka Sudan Kusini na Nigeria wamesema utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF umefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na dhamira ya dhati inayoonyeshwa na serikali katika kupambana na umaskini kwa kuwashirikisha wananchi.

Akitoa maelezo kwa Wageni hao,Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Ladislaus Mwamanga amesema mafanikio ya shughuli za Mpango yametokana kwa kiasi kikubwa na ushirikishaji wa Wananchi tangu katika hatua za awali hadi sasa,huku akiipongeza Serikali kwa kuratibu kwa ufanisi utekelezaji wa shughuli za Mpango huo.

Ametaja baadhi ya mafanikio ya Mpango kuwa ni kuhamaisha walengwa wa Mpango kufanya kazi za uzalishaji mali kwa kutumia ruzuku wanayoipata na kuboresha makazi yao kwa kujenga nyumba bora, huku msisitizo pia ukiwekwa katiamsekta za elimu, afya na lishe hususani kwa watoto na mama wajawazito.

Ujumbe huo utapata fursa ya kutembelea mkoa wa Dar es salaam na Pwani ambako utakutana na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kujionea namna wanavyonufaika na Mpango huo.

Zifuatazo ni picha za tukio hilo.

pic1

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akizungumza na wageni kutoka Sudan Kusini na Nigeria (hawapo pichani) kwenye ukumbi wa mikutano wa TASAF jijijini Dar es salaam,wageni hao wako nchini kujifunza namna TASAF inavyotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.

pic2

Mmoja wa wageni kutoka Sudan Kusini  akizungumza kwenye ukumbi wa mikutano wa TASAF jijini Dar es salaam juu ya azma ya serikali yao kujifunza utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kwenda kuutekeleza nchini kwao.

pic3

Mmoja wa wageni kutoka Nigeria akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mafunzo ya namna TASAF inavyotekeleza shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini uliohudhuriwa na wataalamu kutoka Sudan Kusini na Nigeria.

pic4

Wajumbe kutoka Sudan Kusini,Nigeria,na baadhi ya Watumishi wa TASAF makao makuu wakiwa katika picha ya pamoja nje ya ofisi za TASAF jijini Dar es salaam.

 

 

USAID YAPONGEZA MCHANGO WA MFUKO WA MAENDELEO YA JAMII-TASAF KATIKA KUBORESHA MAISHA YA WANANCHI.

User Rating: 0 / 5

Star InactiveStar InactiveStar InactiveStar InactiveStar Inactive

Mkurugenzi  Mkazi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa -USAID, Andy Karas amefanya ziara katika mkoa wa Kagera na kukagua shughuli zinazofanywa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF na kuridhishwa na maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani humo.

Akiwa katika kijiji cha Mishenyi kata ya Butelankuzi wilaya ya Bukoba Vijijini ,Mkurugenzi Mkazi huyo wa USAID alitembelea Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambako alijionea namna Walengwa hao walivyoboresha makazi yao kwa kujenga nyumba bora kwa kutumia ruzuku itolewayo na TASAF .

Aidha Karas alipata ushuhuda wa Walengwa namna wanavyotumia ruzuku hiyo katika kuboresha huduma za elimu na afya kwa kaya zao huku pia wakitilia mkazo suala la uanzishwaji wa miradi midogo midogo ya uzalishaji mali kwa lengo la kujiongezea kipato chao.“huu ni mwelekeo sahihi na unaopaswa kuungwa mkono na wapenda maendeleo kama USAID kwani unatekelezwa kwa misingi endelevu” alisisitiza Mkurugenzi Mkazi huyo wa USAID.

Katika hatua nyingine Mkurugenzi Mkazi huyo wa USAID alikagua miradi na bidhaa mbalimbali inayotekelezwa na Walengwa wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Mishenyi kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato na kukuza uchumi wao. Miongoni mwa bidhaa hizo ni mbuzi, kuku,vikapu, mayai,vikapu na Mikungu ya ndizi.

Nao Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji hicho cha Mishenyi waliipongeza serikali kwa kubuni Mpango huo kupitia TASAF ambao wamesema umesaidia kurejesha utu wao kwani hapo awali waliishi katika hali ya ufukara na sasa wanaona nuru ikiwarejea kwa kuanza kumiliki mali na kumudu kuendesha maisha yao kaya zao.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Miradi wa TASAF,Amadeus Kamagenge,aliwahakikishia walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kote kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii imeweka mkakati madhubuti wa kuwashirikisha walengwa katika kupunguza umaskini huku mkazo ukiwa ni kwa wao kufanya kazi za uzalishaji mali.

Zifuatazo ni picha za tukio hilo.

 pic1

Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Misaada la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa ,USAID, Andy Karas akikagua moja ya mabanda ya kufugia mbuzi lililoanzishwa na mmoja wa Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, katika kijiji cha Mishenyi wilaya ya Bukoba mkoani Kagera kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato.

pic2

Mkurugenzi  Mkazi wa USAID  Andy Karas  na Mkurugenzi wa Miradi wa TASAF Amadeus Kamagenge wakiangalia bidhaa zilizotengenezwa na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Mishenye kata ya Butelankuzi halmashauri ya wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.

pic3

Mkurugenzi  Mkazi wa USAID  Andy Karas (aliyeshika daftari) akiangalia bidhaa zilizotengenezwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na TASAF  katika kijiji cha Mishenyi  kata ya Butelankuzi wilaya ya Bukoba mkoani Kagera kama njia mojawapo ya kujiongezea kipato na kupambana na umaskini.

pic4

Mkurugenzi Mkazi wa USAID  Andy Karas (wanne kulia )katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa miradi wa TASAF Amadeus Kamagenge (wa pili kulia )nje ya nyumba iliyojengwa na mmoja wa Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kwa kutumia fedha za Mpango huo  katika kijiji cha Mishenye kata ya Butelankuzi wilaya ya Bukoba mkoani Kagera.

pic5

Hapa ni mwendo wa zawadi tu, Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na TASAF katika kijiji cha Mishenye kata ya Butelankuzi wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wakimpatia zawadi mgeni wao Mkurugenzi Mkazi wa USAID baada ya kuzungumza nao na kuwatia moyo wa kufanya kazi ili waweze kuondokana na umaskini.