pic1

Catherine Daudi (35) anaishi katika kijiji cha Iwambi, kilichoko Halmashauri ya Mbeya vijijini. Anaishi na watoto wake watatu na mumewe. Watoto wake wawili wanasoma, mmoja akiwa shule ya awali na mwingine shule ya msingi. Mama huyu ni miongoni mwa watu wanaotoka katika kaya 100 zinazofaidika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaotekelezwa katika kijiji hicho.

Mama huyu anaeleza hali ya maisha yake ilivyokuwa hapo awali katika hali ya kusikitisha sana. Kuna wakati alishindwa kujizuia, anaishia kulia sana. Anasema alifiwa na mume ambaye alimwacha na watoto. Kuwatunza watoto hao ilikuwa kazi ngumu sana kwake. Alikuwa akipata mlo mara moja tu kwa siku ambao ulikuwa na mchanganyiko wa ugali na maharage. Ili watoto waende shule alilazimika kukopa fedha kutoka kwa wenye maduka hapo kijijini. Lakini alilazimika kurudisha madeni hayo kwa kupewa kazi ngumu na nyingi kuliko fedha alizokopa. Hakuwa na jinsi bali kufanya hizo kazi ili aendelee kulea watoto wake.

pic2

Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ulipoingia katika kijiji chao, kaya yake ilikuwa miongoni mwa kaya zilizotambuliwa na kuandikishwa ili kupata ruzuku ya kila mwezi. Naam, hadi sasa amepata mikupuo ya malipo mara kumi. Fedha hizo zimemsaidiaje? "Kwa kweli, fedha hizi zimenisaidia sana", Catherine anasema. Awali, alitumia fedha yote aliyopata kununua mahitaji ya watoto wa shule na chakula. Lakini alipofikiria siku za baadaye, alianzisha mradi wa kutengeneza na kuuza maandazi hapo kijijini. Alianza na shilingi elfu kumi tu. Alichagua kibanda kilichopo njia panda kuwa sehemu yake ya biashara ambapo watu wengi wanapita na si mbali na shule, ili iwe rahisi kwa wapita njia na wanafunzi kununua maandazi hayo kwa urahisi. Kwa sasa anatumia vyumba viwili kwa ajili ya kupika na kuuza maandazi yake.

Anapata faida kiasi gani kutokana na biashara hiyo? Catherine anasema kila siku anatumia gharama ya shilingi elfu hamsini kutengeneza maandazi. Akiuza, kwa wastani anapata faida ya shilingi elfu kumi kila siku. Hii ina maana kwamba anapata kati ya shilingi elfu hamsini hadi themanini kwa wiki. Aidha, Catherine anauza chai asubuhi kwa watu ambao wanahitaji na hivyo kuongeza kipato zaidi. "Wakati wa malipo, nautumia kama fursa maalum ya kipata fedha zaidi kwani napika maandazi mengi zaidi na wenzangu wananunua yote.

pic3

Catherine anasema fedha anazopata kutokana na biashara yake imemwezesha kujenga nyumba ya vyumba vinne na kuezeka kwa mabati na kusakafia kwa saruji. Hilo limemfanya kuhama kutoka nyumba yake ya awali ya chumba na sebule ambayo iliezekwa kwa nyasi. Pili, yeye na familia yake wanapata milo mitatu kwa siku ambapo wanapata nyama au samaki mara tatu kwa wiki. Watoto wake wanaenda shule wakiwa wameshiba; kwa hivyo wanaweza kufuatilia masomo yao vizuri. Maendeleo yao shuleni ni mazuri.

Aidha Catherine anasisitiza kwamba TASAF imemfanya aonekane mtu katika watu maana ilimuwezesha kupata mume kwa mara nyingine. "Mume wangu ni fundi mwashi, pesa anazopata kwenye kazi zake tunaunganisha na zangu kutoka kwenye biashara na kufanya vitu vya maendeleo.

Ana neno gani kwa Serikali na Wadau wa Maendeleo? "Kwanza naishukuru serikali kwa kuanzisha Mpango huu; ni Mpango muhimu sana kwa watu maskini kama sisi. Ukweli mpango unatutoa sana. Ukijiongeza unafanya mambo ya maendeleo kwelikweli. Unatuwezesha kusomesha watoto wetu. Tunaiomba sana serikali ifanye kila jitihada kuufanya Mpango huu uwe wa kudumu", ndivyo Catherine anavyosisitiza.

Kuhusu uwezo wa kujiendesha kama angeondolewa kwenye Mpango, Catherine anasema kwa hapo alipofikia anaweza kuendelea bila kuhitaji msaada wowote. Anategemea kuanzisha miradi mingine ya maendeleo ili aweze kupata fedha zaidi.

pic4