Habari
Wajumbe wa Taasisi ya Ladies of New Millennium waipongeza TASAF kwa utekelezaji bora wa Shughuli za Mpango.

Katika hatua inayoonesha dhamira ya dhati ya wanawake viongozi kushiriki katika maendeleo ya jamii, taasisi ya Ladies of New Millennium ikiongozwa na Mama Tunu Pinda imefanya ziara mkoani Mwanza kutembelea miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF inayotekelezwa chini ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini PSSN.
Wanawake hao, waliotoka katika nyanja mbalimbali za uongozi, walifanya ziara katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza ambapo walishuhudia mafanikio ya mpango huo katika maeneo ya elimu, ujasiriamali na nishati safi ya kupikia.
Wakiwa katika Shule ya Sekondari ya Igogwe, waliona maboresho ya miundombinu ya elimu yaliyofanikishwa na TASAF, hatua inayowezesha wanafunzi kutoka kaya masikini kupata mazingira bora ya kujifunzia.
vikundi vya wanawake wajasiriamali walioinuliwa kupitia mpango huo kwa mafunzo na mikopo midogo, hatua iliyowaimarisha kiuchumi.
Kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha nishati salama na rafiki kwa mazingira, taasisi hiyo iligawa mitungi ya gesi kwa walengwa, wakisisitiza kuwa afya ya familia na mazingira bora ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu.
Katika ziara hiyo, wajumbe hao walikutana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Balandya Mayuganya, ambaye aliwapa taarifa za utekelezaji wa mpango huo katika mkoa huo na mafanikio yaliyopatikana.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Shedrack Mziray, Mkurugenzi wa Mifumo,Tathmini na Mawasiliano Bw. Japhet Boaz, alieleza kuwa zaidi ya kaya milioni moja zimenufaika na mpango huo katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, afya na ajira za muda,
“TASAF inaendelea kujenga uwezo wa walengwa kushiriki kikamilifu katika maendeleo yao,” alisema. Wajumbe waliotembelea miradi hiyo ni Mama Tunu Rehani Pinda, Asina Kawawa, Blandina Mususa, Suzana Charles Majua na Frida Rugemalira .
Ziara hiyo imeweka wazi kuwa wanawake wana nafasi muhimu siyo tu kama walengwa wa maendeleo, bali kama waratibu, wachochezi na wadau muhimu wa mabadiliko chanya katika jamii