Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yaihakikishia TASAF ushirikiano awamu ya tatu ya Mpango


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuendelea kushirikiana kwa karibu na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF katika kuhakikisha utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ili uwe na mafanikio makubwa zaidi kuliko awamu zilizopita.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, wakati wa mazungumzo na viongozi wa TASAF waliofanya ziara ya kikazi Vuga, Unguja leo Septemba 9, 2025.

Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Abdulla amesema TASAF imekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya wananchi kupitia ruzuku na miradi mbalimbali iliyoanzishwa na kaya masikini nchini.

“Niwatake watendaji wa TASAF kuendelea kutoa elimu kwa wananchi hasa walengwa na wanufaika wa programu, kuhusu masharti, muda wa utekelezaji na sifa za kuingia au kutoka kwenye Mpango, ili kuondoa sintofahamu zinazoweza kujitokeza,” amesema.

Mhe. Abdulla alisisitiza kuwa elimu kwa walengwa ni silaha muhimu ya kupunguza malalamiko na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu namna TASAF inavyotekeleza majukumu yake kwa Awamu husika; huku aliupongeza uongozi na watendaji wa Mfuko huo kwa kuonesha uzalendo na weledi mkubwa licha ya changamoto zinazojitokeza.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shedrack Mziray, amemshukuru Makamu wa Pili wa Rais na Serikali ya Zanzibar kwa kuendelea kushirikiana na TASAF. Amebainisha kuwa kupitia Awamu ya Pili inayotarajiwa kufikia ukomo Septemba 30, 2025, zaidi ya walengwa milioni 1.3 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamenufaika na ruzuku, ajira za muda, na mitaji ya biashara.

“Programu ya Awamu ya Pili imewezesha zaidi ya shilingi bilioni 41.6 kuingia moja kwa moja kwa walengwa, ikiwemo fursa za kujipatia kipato kupitia ajira za muda na mikopo midogo ya kuanzisha miradi ya kimaendeleo. Hii ni hatua kubwa katika kupunguza umasikini na kuongeza ustawi wa kaya nchini”, alisema Bw. Mziray.

Bw. Mziray ameongeza kuwa awamu ya tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini, itakayoanza Januari 2026 na kudumu kwa miaka minne, inalenga kufikia walengwa wapatao 575,000. Programu hiyo itajikita katika maeneo yaliyoathirika zaidi na umasikini na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ikiwawezesha wananchi kupata ruzuku, ajira za muda na afua mbalimbali za Mpango.

Ziara hiyo ya kikazi Zanzibar ilitoa nafasi kwa pande zote mbili, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na TASAF, kujadili mikakati ya kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa mpango unaokuja, ili kuhakikisha manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi maskini yanaimarishwa zaidi na kuchangia ajenda ya kitaifa ya ustawi na maendeleo ya jamii.