Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ni mpango wa serikali uliobuniwa kwa lengo la kupunguza umasikini na kuboresha ustawi wa jamii nchini Tanzania. Mfuko huu ulianzishwa mwaka 2000, unatekelezwa kama mpango wa kinga ya kijamii unaolenga kuwezesha kaya maskini na zilizo hatarini kufanikisha maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
Mpango wa TASAF imekusudiwa kufikia kaya maskini zaidi katika maeneo ya vijijini na mijini, kwa kuwapatia msaada unaohitajika ili kukidhi mahitaji ya msingi na kushiriki katika shughuli za kujiongezea kipato. Kupitia utekelezaji huu, TASAF inalenga kuvunja mzunguko wa umasikini na kukuza maendeleo jumuishi kote nchini Tanzania.
DIRA NA DHAMIRA
Katika utekelezaji wake, TASAF inalenga kubuni na kuendeleza afua endelevu na zenye kuleta usawa wa kijinsia, zinazoshughulikia mizizi ya ukosefu wa usawa kulingana na jinsia, umri na ulemavu.
- DIRA Kuziwezesha na kuzilinda kaya maskini dhidi ya hatari na udhaifu, huku zikisaidia jamii zenye huduma duni kwa ajili ya maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi.
- DHAMIRA: Kupunguza umasikini uliokithiri kwa kutekeleza afua jumuishi za ulinzi wa kijamii kwa kaya maskini na jamii zenye huduma duni kwa kushirikiana na wadau kutatua changamoto zinazoikabili jamii.