Habari
Balozi wa Uingereza apongeza miradi ya TASAF Chamwino

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala TASAF akimkaribisha Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. David Concor alipotembelea Makao Makuu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF jijini Dodoma
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. David Concor akiwa katika picha ya pamoja na watendaji wa TASAF na Maofisa wa Ubalozi wa Uingereza
Balozi wa Uingereza hapa Tanzania David Concar amepongeza mifumo inayotumiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF wakati wa utekelezaji miradi mbalimbali inayolenga kuwainua kiuchumi watanzania.
Balozi Concar ametoa pongezi hizo baada ya kumaliza ziara rasmi katika Kijiji cha Ikombolinga wilayani Chamwino mkoani Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine amezuru baadhi ya miradi inayotekelezwa na TASAF ikiwemo bwawa kubwa la maji ambalo limekuwa mkombozi wa wakazi wa kijiji hicho na kijiji jirani cha Mguba.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. David Concor alipokuwa akizungumza na walengwa wa TASAF (hawapo pichani) katika kijiji cha Ikombolinga, wilayani Chamwino
"Imekuwa fursa nzuri kutembelea kijiji hiki katika Wilaya ya Chamwino hapa Dodoma, nilikuja hapa nikijaribu kuelewa jinsi Mfumo wa Hifadhi ya Jamii wa Serikali ya Tanzania unavyofanya kazi, na nilichojifunza leo kinavutia sana." Amesema Balozi David Concar.
Akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TASAF Godwin Mkisi, Balozi Concar pia ameshuhudia jinsi malipo yanavyofanywa kwa walengwa, lakini pia akapata fursa ya kusikiliza shuhuda za wanufaika wa miradi ya TASAF.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala – TASAF akitoa ufafanuzi kwa Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. David Concor kuhusu utaratibu wa kupokea malalamiko wakati wa zoezi la malipo katika kijiji cha Ikombolinga wilayani Chamwino
"Leo nimeshuhudia wanufaika wanavyoshiriki katika Mpango huu kama wanachama hai wenye ubunifu katika matumizi ya fedha wanazopata na hawakai kusubiri kupokea pesa tu” alisema Balozi.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TASAF Godwin Mkisi aliainisha miradi inayotekelezwa na mfuko huo, pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika mpango wa kunusuru kaya za walengwa ambao una jumla ya wanufaika 1,378,000 waliopo katika vijiji 17,260 vya Tanzania Bara na Zanzibar.
Mkisi ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa kuwa sehemu ya wadau muhimu wa Tanzania katika kufanikisha mpango wa kuwafikia walengwa wa miradi ya TASAF. Serikali ya Uingereza inaunga mkono mpango wa TASAF pamoja na washirika wengine 14 wa maendeleo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikombolinga, Mashaka Mchiwa ameishukuru serikali kwa kusaidia maendeleo ya wakazi wa eneo lake, akitolea mfano bwawa kubwa la maji.
"Mbali na sisi, sehemu nyingine inayonufaika na Bwawa hili ni kijiji cha karibu kiitwacho Mguba ambako wakazi wake wanapanga foleni kutafuta maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali." Alisema Mashaka Mchiwa.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Mhe. David Concor na viongozi mbalimbali katika bwawa la maji Nyikani kijiji cha Ikombolinga wilayani Chamwino