Habari
TASAF yabainisha mafanikio mpango wa kupunguza umaskini
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Shedrack Mziray ameeleza mafanikio makubwa ya Mradi wa Kupunguza Umaskini Awamu ya Nne (TPRP IV) uliokamilika Desemba 2025. Amesema mradi huo wa kimkakati umefanikiwa kutekeleza miradi mingi ambayo imekuwa mkombozi kwa jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari wilayani Karatu mkoani Arusha, Mziray amesema mradi huo umechangia kwa kiwango kikubwa kuendeleza ajenda ya maendeleo ya taifa, hususani kupunguza umaskini, kuboresha huduma za kijamii, na kuwezesha jamii nchini.
“Tangu kuanza kwa mradi huu Januari 2020, TPRP IV imejikita kimkakati katika kupunguza umaskini katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Njombe, Geita na Simiyu.
“Lengo kuu lilikuwa kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii na fursa za kuongeza kipato, hii imefanyika kwa kupitia ujenzi na ukarabati wa miundombinu lengwa, mradi umewezesha ujenzi na ukarabati wa madarasa, vituo vya afya na vyanzo vya maji ambavyo sasa vinahudumia kaya za walengwa pamoja na jamii kwa ujumla.
“Uwekezaji huu umeongeza upatikanaji wa huduma, umepunguza umbali wa kufikia huduma za afya na maji, na kuimarisha mazingira wezeshi kwa ustawi wa jamii. Mradi pia umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha ustahimilivu wa kiuchumi,” amesema.
Akieleza zaidi amesema kaya zilisaidiwa kutanua wigo wa vyanzo vya kipato kupitia shughuli kama ajira binafsi katika sekta mbalimbali ikiwemo za kilimo, ufugaji na shughuli nyingine za uzalishaji.
Amefafanua matokeo yake, familia nyingi zimeongeza kipato cha kaya, kuboresha usalama wa chakula na kuimarisha uwezo wa kukidhi mahitaji ya msingi.
“Tathmini za hivi karibuni zinaonesha kuwa mradi huu (TPRP IV) umenufaisha kaya takriban 200,007 kwa kiwango cha mwitikio wa asilimia 96.7, jambo linaloonesha wigo mpana na athari chanya za afua za mradi.
“Mojawapo ya mafanikio makubwa ni kukuza usawa wa kijinsia na kuunga mkono elimu ya wasichana. Ujenzi wa mabweni, vyoo na madarasa umeongeza uandikishaji, kuboresha udumishaji wa wanafunzi shuleni, na kupunguza mimba za utotoni,” ameleza.
Pia, amesema hatua hizo zimechangia kuboresha matokeo ya kielimu na kuongeza fursa kwa wasichana. Msisitizo wa ushirikishwaji wa jamii umejenga uwajibikaji wa pamoja na uendelevu, kuhakikisha rasilimali zinaendelea kufanya kazi na kutunzwa hata baada ya mradi kukamilika.
