Historia
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilianza kutekeleza Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuanzia mwaka 2000, ikiwa ni moja ya mbinu za kutokomeza umasikini ambazo pia zilisaidia ajenda ya ugatuaji wa madaraka. Katika kipindi cha 2009 - 2012, TASAF ilifanya majaribio ya uhawilishaji fedha taslimu kwa masharti. (CCT). Majaribio hayo yalifanyika katika Wilaya za Kibaha, Bagamoyo na Chamwino za Tanzania Bara.
Tathimini ya matokeo ya majaribio hayo ilionesha mafanikio makubwa katika sekta za afya, elimu na kuongezeka kwa rasilimali za kaya. Kutokana na misingi hii afua za TASAF zilizokuwa zinatumika hapo awali zimebadilika kuwa mfumo wa kinga ya jamii tangu mwaka 2012 kwa utekelezaji wa Awamu ya Kwanza ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (PSSN I)
Madhumuni ya PSSN I ilikuwa ni kuziwezesha kaya masikini kuongeza vipato na fursa za kujikimu. PSSN I (2013 – 2019) ilifikia lengo kwa kusajili kaya milioni moja kutoka vijiji 10,000 kwenye Mamlaka 161 za eneo la Mradi (Jiji/Manispaa/Wilaya/Halmashauri za Miji na Unguja na Pemba kwa upande wa Zanzibar)
Kaya zilizolengwa zilinufaika kupitia uhawilishaji fedha wa msingi, na uhawilishaji fedha wa masharti ya watoto kuhudhuria kwenye vituo vya afya na shuleni. Pamoja na uhawilishaji fedha, walengwa 300,000 kutoka maeneo ya utekelezaji 44 walitekeleza miradi ya jamii 3500. SEhemu ya kukuza uchumi wa kaya ilifanyiwa majaribio katika maeneo ya utekelezaji 8 ambapo vikundi 5,000 vya kuweka na kukopa vyenye wanachama 74,000 viliundwa.
Kupitia sehemu ya kuimarisha mifumo ya taasisi, usimamizi wa utekelezaji wa shughuli za mpango katika ngazi za Taifa, Maneo ya Utekelezaji, Kata na Jamii unafuatiliwa kwa kutumia mfumo wa usimamizi wa taarifa (MIS). Walengwa wanaendelea kupokea malipo yao kwa fedha taslimu wakati huo huo taratibu za kulipa kwa njia ya kielektroni zinafanyika kwa awamu hadi hapo maeneo yote yatakapofikiwa. Aidha mifumo ya kushughulikia malalamiko na wa ufuatiliaji wa shughuli za Mpango umeendea kutoa taarifa zinazotumika kupanga na kutekeleza shughuli mbali mbali