Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

TASAF yapongezwa kwa utekelezaji thabiti wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini


Kamati ya Kudumu ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imezipongeza Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Zanzibar kwa kuendelea kuboresha maisha ya wananchi wa pande zote mbili kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaofanywa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF.

Wajumbe wa kamati hiyo wamesema kwa upande wa Zanzibar, TASAF imezifikia kaya 53,000 ambazo zimenufaika na hali za maisha yao zimeimarika tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Akizungumza wakati wa ziara iliyofanyika katika ofisi za TASAF jijini Dar es Salaam Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mwanaasha Hamis Juma amesema Mpango wa kunusuru Kaya Maskini umewezesha kupungua kwa hali ya umaskini uliokithiri kwenye kaya za walengwa.

"Tunafurahi kwamba  TASAF imesaidia kaya masikini na kuboresha miundombinu lakini kuwezesha kaya masikini zilizoandikishwa kwenye mpango huu  kunufaika kwa kuwa na shughuli za ujasiliamali na kuwa na kipato endelevu  kwa ajili ya kumudu mahitaji ya kila siku,” alisema.

Mhe Mwanaasha aliongeza kwamba; "Kamati ya Bajeti imekuwa ikiona maendeleo na taarifa mbalimbali kuhusu TASAF kwa hiyo leo tumekuja kuona mafanikio na changamoto, tumefarijikwa kuwa mafanikio ni mengi”.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Shedrack Mziray amesema wamepata bahati ya kutembelewa na Kamati ya Kudumu ya Bajeti Baraza la Wawakilishi Zanzibar ambapo amefafanua kuwa Mpango wa TASAF unatekelezwa katika pande zote mbili kwa maana ya Zanzibar na Bara.

Alisema kuwa ziara hii ni sehemu ya maandalizi ya vikao vya bajeti kwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar linalotarajiwa kuanza vikao vyake wiki ijayo.

Kwa upande wa Zanzibar, Tasaf inatekelzwa chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, hivyo kamati hiyo imetembelea taasisi zinazotekeleza miradi mbalimbali ya maelendeleo kwa pande zote mbili za Muungano.

"Tumewaelezea maendeleo ya mradi na kwa upande wa Zanzibar tunashugulika na walengwa 53,000 na ujumbe mkubwa ambao tumeupeleka ni kwamba Mpango huu umekuwa unatekelezwa kuanzia mwaka 2021, utahitimishwa mwezi semptemba mwaka huu 2025,” alisema

"Kwahiyo kwa sasa tunawaelewesha wananchi kuhusu ruzuku ambazo tunawapatia kila mwezi pamoja na shughuli nyingi ambazo wamekuwa wakizifanya walengwa ruzuku zitasitishwa kuanzia Septemba mwaka huu.

Mziray aliitarifu kamati hiyo kwamba  kwa sasa serikali inafanya maandalizi ya kuanza  programu mpya ambayo inatarajiwa kuanza baada ya kukamilika kwa programu ya sasa.

Hivyo amewaomba wananchi wawe na matumaini kwa mradi utaendelea baada ya kukamilisha mchakato wa programu mpya na watakwenda kutambua ambao hawakufikiwa katika awamu ya sasa hivyo watakuwa na walengwa wapya na wataendelea na taratibu kama ambavyo mradi mpya utaandaliwa.

Zaidi ya kaya 9,400 zilifanyiwa tathimini na kuonekana zimeboreka kimaisha hali zao kiuchumi zimekuwa nafuu, hivyo walisitishiwa kupata ruzuku Julai mwaka 2024.

"Kwahiyo wameridhishwa na utekelezaji na wameipongeza TASAF kwa kazi nzuri wanaiyofanya kwa upande wa Zanzibar na wako tayari kuishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili nayo iweze kusimamia vizuri mradi na kuongeza bajeti katika mradi huu kwa kipindi kipya kinachokuja,"amesema Mziray.