Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Watoto kutoka Kaya za Walengwa kuunganishwa katika Program za Kukuza Ujuzi


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameshauri TASAF kufanya mawasiliano na Mpango wa Kukuza Ujuzi unaoendeshwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Wizara ya Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu kuona jinsi ya kuwaunganisha na program hiyo watoto wanaotoka katika kaya zilizoko kwenye Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa ambao hawakuweza kuendelea na masomo baada ya kumaliza elimu ya msingi, sekondari na kidato cha sita ili kupata ujuzi utakaowawesha kujiajiri.

Waziri Mhagama amesema hayo leo Jumatano Februari 9, 2022 alipotembelea Makao Makuu ya Mfuko wa Maendeleo ya  Jamii - TASAF jijini Dodoma na kupata taarifa ya shughuli za Mfuko huo.

Waziri Mhagama alisema hayo baada ya kupata taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga kuwa TASAF imeingia makubaliano na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ili kutoa mikopo kwa wanafunzi waliodahiliwa na kuwa na vigezo vya kujiunga na elimu ya juu wanaotoka kaya za walengwa wa TASAF. Bodi hiyo ya mikopo hutoa mikopo kwa asilimia 100 kwa wanafunzi wanaotoka Kaya za walengwa waliokidhi vigezo vya kujiunga na elimu ya juu.

Mwamanga amesema mwaka jana jumla ya wanafunzi 1,200 kutoka kaya za walengwa walipata mkopo kwa asilimia 100 na mwaka huu wanafunzi wapatao 2,500 wanatarajiwa kupata mkopo kutoka Bodi hiyo.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akilakiwa na mwenyeji wake Mkurugenzi wa TASAF Ladislaus Mwamanga

 

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga akimpatia zawadi mgeni wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama

Amesema katika mpango huo wanafunzi hufundishwa ujuzi mbalimbali na kuweza kujiariji katika shughuli mbalimbali. Amesema vijana kutoka kaya za walengwa wakipitia utaratibu huo wataweza kusaidia kaya zao kujikwamua mapema zaidi kutoka katika umasikini.

Mhe. Mhagama amesema mradi wa TASAF ni wa mfano kwa kuwa unamfikia mwananchi  wa chini kabisa katika pande zote mbili za Muungano.