Habari
Halmashauri 23 kupata magari mapya kwa ajili ya shughuli za TASAF

Halmashauri 23 zinazotelekeza shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF zinapata mafunzo ya matumizi ya magazi ambayo yatakabidhiwa kwao 30.9.2022. Magari hayo mapya aina ya Toyota Land Cruiser ni sehemu ya magari ambayo yametolewa na Serikali kwa ajili ya shughuli za Mfuko wa Maendeeo ya Jamii TASAF. Mnamo Aprili 2022, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alikabidhi mkupuo wa kwanza ya magari 123 yaliyokwenda kwenye baadhi ya Halmashauri zinazoendesha shughuli za TASAF Tanzania Bara, Unguja na Pemba.
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TASAF Bw. Godwin Mkisi, alisema magari hayo 23 ni mkupuo wa pili wa shehena ya magari iliyoagizwa kwa ajili ya shughuli za TASAF na kwamba mkupuo wa mwisho wa magari 35 unatarajiwa kukabidhiwa kwa wahusika mwezi Oktoba 2022 na hivyo kukamilisha zoezi la kukabidhi magari yote 241 ambayo yamenunuliwa kwa ajili ya shughuli za mradi wa TASAF katika Halmshauri zote 184, TASAF Makao Makuu, TAMISEMI, Unguja na Pemba
Mkurugenzi wa Fedha na Utawala Bw. Godwin Mkisi akitoa neno kwa maafisa usafirishaji na madereva kabla ya kumkaribisha Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga wakati wa zoezi la kukabidhi magari kwa Halmashauri 23 katika ukumbi wa mikutano ofisi za TASAF – Dar es Salaam
Akifungua mafunzo hayo yaliyowahusu madereva na maafisa usafirishaji wa halmashauri hizo 23, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF bwana Ladislaus Mwamanga alisema kwamba malengo ya mafunzo hayo ni kuwakumbusha madereva na maafisa usafirishaji masuala muhimu kuhusu matumizi ya magari hayo. “Magari haya yanakabidhiwa kwenye halmashauri zenu kwa ajili ya shughuli za TASAF. Yanaweza kutumika kwenye shughuli nyingine za halmashauri pale kunapokuwa na shughuli nyingine za kiujumla kama ilivyokuwa wakati wa sensa lakini kipaumbele ni shughuli za TASAF. Isitokee shughuli za TASAF zikashindwa kufanyika kwa kukosekana usafiri”
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga akitoa maelezo na maagizo kwa maafisa usafirishaji na madereva (hawapo pichani) wa Halmashauri zinazochukua magari katika ukumbi wa mikutano ofisi za TASAF – Dar es Salaam
Bw. Mwamanga pia aliwakumbusha madereva na hasa maafisa usafirishaji kwamba magari hayo yamepangiwa kufanya kazi katika eneo la kijografia la Halmashauri hizo tu na endapo kutakuwa na ulazima wa gari kusafiri nje ya eneo hilo taratibu za kutoa gari nje ya eneo la mradi zifuatwe ikiwa ni pamoja na kuomba kibali na taarifa zitolewe. Magari hayo yamefungwa ving’amuzi vinavyoonesha maeneo ambayo gari hilo lipo.
Mkurugenzi Mwamanga pia alisisitiza utunzaji wa magari hayo ili yaweze kudumu na kwa muda mrefu ikiwa ni kufanya service kwa wakati, kuhakikisha mafuta na vilainishi vitakavyotumika ni salama na vilivyoidhinishwa ili kuzuia uharibifu.
Aidha Mwamanga alisisitiza kwamba halmashauri ambayo haitakabidhi gari la zamani basi haitapata gari jipya sambamba na maelekezo yaliyotolewa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan wakati alipokabidhi awamu ya kwanza ya magari 123.
Baadhi ya madereva na maafisa usafirishaji wakimsikiliza Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga (hayupo pichani) wakati wa zoezi la kukabidhi magari kwa Halmashauri 23 katika ukumbi wa mikutano ofisi za TASAF – Dar es Salaam
Halmashauri 23 ambazo zitakabidhiwa magari mapya baada ya madereva na maafisa usafirishaji kupata mafunzo ni Halmashauri za Wilaya za Hai, Mwanga, Babati, Kiteto, Singida, Biharamulo, Butiama, Bahi, Uvinza, Igunga, Sikonge, Lindi, Masasi, Nanyamba, Mbinga, Nsimbo, Muheza, Mpanda, Sumbawanga na Momba. Zingine ni Halmashauri za Mji Kahama na Kibaha, na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.