Habari
TASAF ilivyosaidia wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Mkoani Mbeya

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF umetumia zaidi ya shilingi bilioni 68.6 kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika mkoa wa Mbeya kuanzia mwaka wa fedha 2021/22 hadi 2024/25.
Fedha hizo zimenufaisha jumla ya kaya 37,789 katika Halmashauri Saba za mkoa huo ikiwemo Busokelo, Chunya, Kyela, Mbarali, Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na Rungwe.
Kati ya fedha hizo, kiasi cha shilingi bilioni 2.8 zilitolewa kama ruzuku ya uzalishaji ili kusaidia kaya kuanzisha shughuli za uzalishaji mali katika halmashauri nne ambazo ni Jiji la Mbeya, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Chunya na Rungwe. Fedha hizi zinalenga kuwasaidia walengwa kujenga maisha endelevu na kuvunja mzunguko wa umaskini.
Hayo yalibainishwa katika ziara ya siku mbili ya ufuatiliaji mkoani Mbeya iliyofanywa na menejimenti ya TASAF pamoja na Wadau wa Maendeleo wakiongozwa na wawakilishi kutoka Benki ya Dunia na Ubalozi wa Uswisi. Ujumbe huo ulitembelea jamii mbalimbali kujionea matokeo ya moja kwa moja ya utekelezaji wa mpango.
Timu ya TASAF ilikuwa ikiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Bw. Shedrack Mziray, huku Wadau wa Maendeleo wakiongozwa na Bi. Claudia Zambra, kutoka Benki ya Dunia.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bw. Mziray alisema mfuko umefurahishwa na jitihada kubwa zilizofanywa na walengwa ambao wametumia vyema msaada waliopata ili kuboresha maisha yao.
“Tumefurahishwa na hatua kubwa iliyofikiwa na walengwa. Wengi wao wameweza kuboresha hali za uchumi wa kaya zao kutoka kwenye changamoto walizokuwa wanapitia awali. Hii inaonyesha wazi kuwa mpango wa kunusuru kaya maskini unatoa matokeo halisi kwa walengwa,” alisema.
Mnufaika Edna Mbesu alisema kuwa kabla ya mpango huo kutekelezwa, hakuweza kugharamia mahitaji ya shule ya watoto wake. Alikuwa na kifua kikuu ambacho kilisababisha mikono yake kupooza, na hivyo kufanya maisha kuwa magumu kifedha.
“Nilileta watoto wangu kwa kukusanya kuni, na baadhi ya siku tulilala njaa. Baadaye, TASAF ilisaidia kupunguza gharama za maisha. Nilianzisha biashara ndogo ya kuongeza kipato na hatimaye niliweza kuweka akiba ya kutosha kununua mabati ya nyumba yangu,” alisema Edna.
Kwa upande wake, Japhary Winga alieleza shukrani zake kwa mpango huo kwa kumuwezesha kupata mkopo wa elimu ya Juu kupitia barua ya utambulisho hivyo akapata mkopo kwa asilimia mia moja.
“Sasa mimi ni mhitimu mwenye shahada ya Sanaa ya Elimu kutoka Chuo Kikuu Katoliki cha Mbeya. Nashukuru sana kwa sababu awali familia yangu haikuweza kumudu gharama hizi, hali ambayo ilikuwa inazima ndoto zangu,” alisema.
Ujumbe huo pia ulipata nafasi ya kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bw. Beno Malisa, ambaye aliipongeza TASAF kwa mchango wake katika kuboresha maisha ya familia zenye mazingira magumu mkoani humo.
“Tumeona athari chanya za miradi ya TASAF katika jamii zetu. Familia ambazo awali zilikuwa zikihangaika kupata mahitaji ya msingi sasa zinaweza kuwapeleka watoto shule, kupata huduma za afya na hata kuanzisha biashara ndogondogo. Hili ni jambo kubwa sana na nawapongeza TASAF na wadau wake kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kupambana na umaskini,” alisema Bw. Malisa.
Alisisitiza viongozi wa serikali za mitaa na wanajamii kuendelea kushirikiana kwa karibu na TASAF ili kuhakikisha mpango huu unawafikia kaya zote lengwa na kutimiza malengo yaliyokusudiwa.
Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unafadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Wadau wa Maendeleo. Mpango huu unatoa ruzuku ya fedha taslimu, fursa za miradi ya ajira kwa muda, pamoja na msaada wa kipato kwa kaya maskini na zilizo hatarini. Lengo lake kuu ni kuimarisha ustahimilivu wa kaya, kukuza maendeleo ya rasilimali watu na kupunguza umaskini wa muda mrefu.