Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Kamati ya Bunge yashuhudia jinsi TASAF inavyogusa maisha


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria inatembelea miradi inayotekelezwa chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF katika mikoa ya Iringa, Njombe na Ruvuma na kujionea jinsi Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa unavyogusa maisha ya wanufaika wake.

Katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, katika kijiji cha Ibumila Kamati iliona mradi wa shamba ya miti ya parachichi unaotekelezwa na wanufaika chini ya mradi wa Ajira za Muda wenye lengo la kuwapa ujuzi walengwa hao katika kilimo cha parachichi na pia kuwaongezea kipato.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Joseph Mhagama (wa tatu kutoka kushoto) pamoja na wajumbe wa kamati hiyo wakikagua Mradi wa shamba la Parachichi lenye miti 231 uliotekelezwa na walengwa wa TASAF katika Kijiji cha Ibumila Kata ya Mgama Mkoa wa Iringa, kushoto kwake ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete

Akizungumza katika shamba hilo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (MB) alielezea kufurahishwa na kipengele cha kuwapa walengwa ujuzi na kueleza kuwa suala hilo linafanya msaada kwa walengwa kuwa endelevu hata watakapoondoka katika Mpango.

Mkoani Njombe, Kamati imetembelea jengo la afya ya Mama na Mtoto lililojengwa kwa Msaada wa TASAF katika Hospitali ya Mji wa Njombe, na kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la watoto njiti kukosa huduma stahiki.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria yatembelea Mradi wa Ujenzi wa wodi iliyokamilika ya mama na mtoto pamoja na chumba maalumu cha kinamama wanaojifungua watoto njiti kupatiwa huduma bora wao pamoja wa watoto kwenye hospitali ya Kibena iliyopo Mtaa wa Kibena, Kata ya Ramadhani katika Halmashauri ya Mji wa Njombe

Kwa mujibu wa Mganga Mfawidhi wa Wilaya, Dkt. Jabir Juma, katika hospitali hiyo akinamama 300 hujifungua hapo kila mwezi huku akina mama kati ya mmoja na kumi na tano hujifungua kwa njia ya kawaida kila kila siku wakati akina mama kati ya nane na tisa hujifungua kwa njia ya upasuaji.

Amesema watoto kati ya wawili au watatu huzaliwa njiti kila siku na kufanya idadi ya watoto kati ya 20 na 26 kwa mwezi.

Kamati hiyo pia inatembelea mradi wa stendi ya mabasi katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea ambao pia ni moja ya miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na TASAF.

Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria ikitembelea stendi ya mabasi katika kijiji cha Lundusi,Kata ta Peramiho

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama (MB), kwa niaba ya Kamati yake, ameipongeza TASAF kwa kuibua miradi inayojibu changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi na kugusa maisha yao moja kwa moja.