Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Kaya za Walengwa 174,586 kuhitimu TASAF


Kaya za walengwa 174,586 ambao wananufaika na ruzuku kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF wanatarajiwa kuhitimu kutoka Mfuko huo na hivyo kukoma kupokea ruzuku ifikapo mwezi Januari 2023. Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga aliyasema hayo Jijini Dodoma leo kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika kwenye ofizi ya TASAF Dodoma.

Mkurugenzi amezungumza kwamba kaya hizo ni kati ya kaya 1,371,038 zinazohudumiwa na TASAF. Kulingana na maelezo ya Mwamanga, kaya hizo zilifanyiwa uhakiki wa kutathmini hali za ustawi wa maisha yao na kubainika kwamba zimeimarika kiuchumi na zinaweza kuendesha maisha yao bila ya kutegemea ruzuku. Kaya kupitia shughuli zao mbali mbali zina vitega uchumi na biashara zinazoongeza pato la kaya zao na hivyo kukosa tena vigezo vya kuendelea kupokea ruzuku.

Kati ya kaya hizo, kaya 16,490 zinahitimu kutoka kwenye Mpango baada ya kupokea ruzuku ya uzalishaji kupitia program ya kukuza uchumi wa kaya. Ruzuku hii huwezesha kaya ya walengwa kuanzisha mradi endelevu ambao utawezesha kaya kuwa na kipato cha uhakika. Kaya zilizopata ruzuku ya uzalishaji ni kutoka Halmashauri za wilaya ya Bagamoyo, Kibaha,  Lindi, Chalinze na katika Manispaa za Mtwara na Lindi na kutoka Unguja kwa upande wa Zanzibar. Utaratibu wa kutoa ruzuku za uzalishaji ni mkakati wa kuzitoa kwenye Mpango kaya ambazo zimejiimarisha kiuchumi na utaendelea kwenye maeneo mengine ya utekelezaji.

Kwa mujibu wa Mwamanga, utaratibu wa kuziondoa kaya ambazo zimetoka kwenye umaskini uliokithiri na kuimarika kiuchumi ni endelevu na kwamba kundi la Pili la Kaya 223,418 ambazo nazo zimeimarika kiuchumi zinatarajia kuondolewa kwenye Mpango ifikapo Septemba 2023 na kaya hizi zitapewa taarifa rasmi ifikapo mwezi Machi 2023.