Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Mafunzo ya Uundwaji Vikundi vya Kuweka na Kuwekeza kwa Wakufunzi wa Kitaifa


Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeandaa mafunzo ya mpango wa kuweka na kuwekeza kwa kaya za walengwa yatakaofanyika kwa siku tano mkoani Morogoro, kwa maofisa ufuatiliaji wa ngazi za halmashauri kote nchini. Maafisa ufuatiliaji hao wamegawanywa katika makundi mawili ambayo yatajengewa uwezo kuanzia Septemba 20 hadi Septemba 24, 2021 na kundi la pili litajengewa uwezo kuanzia tarehe Septemba 27 hadi Octoba 1 2021.

Mpango wa kuweka na kuwekeza kwa kaya za walengwa ni moja ya sehemu za mpango wa kunusuru kaya za walengwa unaotekelezwa na TASAF. Mpango huo unatekelezwa kwa walengwa baada kuunda vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha, vitakavyo wawezesha kujikopesha na kuanzisha miradi midogo midogo na kuimarisha na kujenga uchumi wa kaya zao.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Mtaalam wa Mafunzo wa TASAF Bi Mercy Mandawa alitoa msisitizo wa kwenda kusimamia uundwaji wa vikundi na kuvifuatilia na kuhakikisha vinaimarika na kuweza kufikia hatua ya kuweza kutoka katika umaskini. Baada ya mafunzo haya wataalamu hawa wataenda kutekeleza mpango huu katika halmashauri zote 184 na vikundi hivyo vitapatiwa mafunzo na kuweza kuandaa katiba, kukamilisha usajili kwa mujibu wa sheria ya vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha ya mwaka 2018 kwa kuwashirikisha maafisa maendeleo ya jamii katika maeneo yao.