Habari
Mfugaji mkubwa wa kuku ajifunza kutoka kwa mlengwa TASAF

Mfugaji mkubwa wa kuku kutoka Chunya, Alex Mwakipesile akistajabia jogoo anayefugwa na mnufaika wa TASAF, Fasness Jaton
Alex Mwakipesile, mfugaji mkubwa wa kuku kutoka Chunya, Mbeya anatarajia kuboresha mbegu ya kuku wake baada ya kupata msaada kutoka kwa mnufaika wa TASAF, Fasness Jaton
Fasness, pamoja na wanufaika wenzake wamefadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF kushiriki Maonesho ya Kilimo kitaifa jijini Mbeya ili kuonesha bidhaa mbalimbali walizozalisha baada ya kupata ruzuku za TASAF.
Mwakipesile, aliyetembelea banda la TASAF alifurahishwa na bidhaa mbalimbali zinazooneshwa na wanufaika hususan kuku chotara wenye uzito wa kati ya kilo tatu hadi tano.
Mfugaji huyo wa kuku alisema anafuga kuku wa kienyeji zaidi ya 300 wilayani Chunya na anakusudia kuboresha kwa kupata mbegu bora zaidi
Kuku wanaofugwa na Fasness wametokana na kuchanganya mbegu ya kuku wa nyama na a mayai aina ya Sasso na Croiler.
Mwakipesile alijifunza kutoka kwa Fasness jinsi ya kutengeneza chakula cha kuku kinachowafaa kuku hao na alinunua mayai kwa ajili ya kutotolesha na kupata vifaranga bora.
“Nitaboresha kuku wangu wa kienyeji na kupata aina hii ya kuku ambao nafikiri watakuwa na tija zaidi…naweza kununua hata mayai 100 kutoka kwako kama unayo,” alisema kabla ya kununua mayai tisa yaliyokuwepo kwenye maonesho na kuahidi kufuata mengine zaidi pindi yatakapopatikana.
Pamoja na Fasness, wanufaika wengine wanaoonesha bidhaa zao katika banda la TASAF ni pamoja na Enos Ngabo anayelima mboga mboga aina ya broccoli na cauliflower, Alon Sanga Joina Sanga na Sarah Mwandima wanaojihusisha na kilimo cha viazi, karoti na ushonaji vikapu pamoja na Msafiri Lwanga anayefuga ng’ombe wa maziwa.
Maonesho ya Nanenane ya mwaka huu yalizinduliwa Agosti 1, 2022 na Makamu wa Rais, Dkt. Isdory Mpango na yanatarajiwa kufungwa Agosti 8, 2022 na Rais Samia Suluhu Hassan