Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Waziri Mhagama apongeza miradi ya miundombinu TASAF


Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais) Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amesema miradi ya miundombinu ya elimu, afya na maji inayojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF ni mfano wa kuigwa na miradi inayotekelezwa na taasisi nyingine.

Ameyasema hayo Jumanne Desemba 13, 2022 alipotembelea ofisi ndogo ya Makao Makuu ya TASAF jijini Dar es Salaam kuzungumza na watendaji wa Mfuko huo kuhusu utendaji wa kazi zao.

Amesema amekagua miradi hiyo sehemu mbalimbali nchini kama vile ujenzi wa zahanati, madarasa na miundombuni ya maji na kujionea kuwa iko katika kiwango bora na kuakisi thamani ya fedha iliyotumika.

Mhe. Mhagama ameipongeza taasisi hiyo kwa kusaidia kaya maskini ambapo nyingi zimeweza kutoka katika umasikini uliokithiri na maisha yao kuwa bora zaidi ambapo zaidi ya kaya 158,000 ziko tayari kuondoka katika mpango.

Ameitaka TASAF kuongeza nguvu za kutangaza mafanikio hayo ya walengwa wanaojitoa kwa hiari ili wananchi wajue zaidi mafanikio ya mfuko huo na wao kupata hamasa ya kufanya vizuri ili hatimae waweze kujitoa kwenye Mpango wa TASAF na kuendesha maisha yao bila kutegemea ruzuku.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na timu ya menejimenti ya TASAF