Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Miradi ya Sh bilioni 9 yatekelezwa Zanzibar


Miradi ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali 13 yenye thamani ya shilingi bilioni 9 imetekelezwa Unguja na Pemba kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii. Miradi hiyo  ni pamoja na ujenzi wa  vituo vya afya,  zahanati na  ujenzi wa kumbi za mitihani katika shule.   

Wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa  ukumbi wa mitihani  katika  shule ya  msingi na sekondari Bambi katika mkoa wa Kusini Unguja Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw Shedrack Mziray  alisem a kuwa miradi hiyo  itarahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi.

Kaimu  Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw Shedrack Mziray akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi la  ujenzi wa ukumbi wa mitihani wa shule ya Msingi na Sekondari Bambi  katika mkoa wa Kusini Unguja

Mgeni rasmi katika hafla hiyo,  Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Tabia Mwitta  Maulid alisema ujenzi wa ukumbi wa mitihani utaepusha msongamano wa wanafunzi wakati wa kufanya mitihani  yao.

“TASAF inafanya kazi kubwa ya kujenga miundombinu mbalimbali na Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi hizi ambazo zinaleta manufaa kwa walengwa na jamii kwa ujumla,” alisema.

Waziri huyo aliwahimiza walengwa wa TASAF na wakazi wa Shehia ya Bambi kutoa ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa mradi ambao unatarajiwa kukamilika Februari, 2024.

Katika ujenzi wa ukumbi huo, TASAF imetoa jumla ya shilingi million 117.5 ambapo hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 68.8 zimetumika na mradi umefikia asilimia 76

Jengo la ukumbi wa mitihani  la shule ya msingi na sekondari Bambi