Habari
Mlengwa TASAF aangua vifaranga kwa siku 17

Sifiaeli Lengaramu (kulia) akiifafanua jambo mbele ya Wajumbe Kamamti ya Uongozi ya TASAF walipomtembela nyumbani kwake Minjingu, Babati mkoani Manyara
Kwa kawaida kuku huatamia mayai kwa siku 21 kabla ya kuangua na kisha kulea vifaranga vyake kwa muda kabla ya kuanza kutaga tena. Lakini hali hii si kwa kuku wanaofungwa na Sifaeli Lengaramu, mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa katika kijiji cha Minjingu, wilayani Babati.
Kutokana na teknolojia aliyoiugundua Lengaramu, kuku wake wanaatamia mayai kwa siku 17 kabla ya kuangua.
Lengaramu, aliyewashangaza wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya Kitaifa ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) waliomtembelea kijijini kwake, hutumia kinyesi cha mbuzi kuongeza joto la ardhi ili kusaidia mayai kutotoa siku nne kabla ya muda wa kawaida.
Lengaramu aliwaelewa wajumbe hao kuwa huchukua kinyesi cha mbuzi na kukifukia mahali ambapo kuku wake wanaatamia mayai na hivyo joto kuweza kutoka juu alipolala kuku na chini kwenye kinyesi na hivyo kukomaza mayai mapema.
Mtindo huo umemfanya Lengaramu kuwa na kuku wengi kwa muda mfupi na hivyo kujiongezea kipato.
Katika kulea vifaranga, Lengaramu amesema amechagua kuku ambao ni hodari wa kulea na wengine walio hodari wa kutaga na kuwapa kazi tofauti.
Sifaeli Lengaramu akiwa na baadhi ya kuku wake nyumbani kwake Minjingu
Vifaranga wakishaanguliwa, mfugaji huyo humpa kuku mwingine kuwalea na hivyo kuku aliyetaga mayai kuwa peke yake na kuweza kutaga mayai mengine.
Mfugaji huyo hutumia dawa za kienyeji za Kimasai kwa ajili ya kutibu kuku wanapopatwa na magonjwa mbalimbali kama vile kideri, mdondo na ndui.
Amesema dawa kienyeji wanazotumia binadamu kujitibu magonjwa mbalimbali ndizo huwapa pia kuku wake.
Wajumbe wa Kamati ya Uongozi ya TASAF wamempongeza mfugaji huyo kwa ubunifu wake na kumtapa kueneza ujuzi huo kwa wananchi wengine.
Mjumbe wa Kamati ya Uongozi Kitaifa ya TASAF, Dkt. Grace Magembe amemshauri Lengaramu kuwa na mpango mbadala endapo kutatokea mlipuko wa ugonjwa kwa kuwa kuku wake ni wengi.