Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

NBS kufanya utafiti matokeo mradi wa OPEC


Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF, Ladislaus Mwamanga (kushoto) na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya  Taifa ya Takwimu (NBS) Dkt Albina Chuwa wakitia saini makubaliano ambapo NBS itafanya utafiti wa mafanikio ya mradi wa miundombinu unaotelekezwa na TASAF na kufadhiliwa na OPEC, katika hafla iliyofanyika Novemba 22, 2022 katika ofisi za NBS jijini Dodoma

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF umeingia makubaliano na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ambapo ofisi hiyo itafanya utafiti wa mafanikio ya mradi wa ujenzi wa miundombinu unaotelekezwa na TASAF na kufadhiliwa na Umoja wa Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi (OPEC).

Hafla ya utiaji saini huo umefanyika Jumanne Novemba 22,2022 katika ofisi za NBS jijini Dodoma na kushuhudiwa na Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi Mhe. Anna Makinda na maofisa wengine.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini huo, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga amesema Mfuko huo unatumia taasisi za ndani ya nchi, hususan NBS kufanya tafiti mbalimbali kuhusu matokeo ya kazi zake kwa kuwa taasisi za ndani zimeonesha uwezo katika kufanya tafiti na kutoa takwimu zenye kiwango kinachokubalika kimataifa.

Mwamanga amesema TASAF imeamua kutumia taasisi za Serikali katika tafiti zake kwa kuwa taasisi hizo zine uwezo na viwango vya kuridhisha.

"OPEC imetoa dola za  kimarekani milioni 50 kwa ajili ya mradi huu, nina imani kwa takwimu za matokeo ya mradi huo zitakazotolewa na NBS, nchi yetu inaweza kupata fedha zaidi," amesema Mwamanga.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dkt. Albina Chuwa ameahidi kuwa taasisi yake itaifanya kazi hiyo kwa ueledi iwa hali ya juu na kutoa matokeo ndani ya muda ulio katika makubaliano.