Habari
Walengwa TASAF wajenga barabara Ruvu Darajani,Uswisi yapongeza

Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika kijiji cha Ruvu Darajani Halmashauri ya Chalinze Mkoa wa Pwani wamefanikiwa kufungua mawasiliano ya barabara katika vitongoji vinne na kupelekea kurashishwa kwa shughuli za usafiri na usafirishaji kijijini hapo.
Mawasiliano hayo yamefunguka baada ya ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara mbili ambapo moja ina urefu wa kilomita 1.8 na nyingine yenye kilomita 1.5 katika vitongoji vya Mlimani, Mwenjeni, Relini na Mkwajuni kwa gharama ya shilingi milioni 26.8
Barabara hizo ambazo zimejengwa na walengwa wa mpango unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF, zimerahisiha muingiliano baina na wana kijiji pamoja na biashara ambazo zinakuza uchumi wa kaya na kijiji kwa ujumla.
Ujenzi wa barabara hizo sambamba na kuimarika kwa uchumi wa walengwa umepongezwa na serikali ya Uswisi ambao ni miongoni mwa wadau wa maendeleo wanaounga mkono utakelezwaji wa afua za kuondoa umasikini nchini.
Akizungumza katika ziara ya kuangalia maendeleo ya walengwa na shughuli wanazozifanya katika kujiingizia kipato, Mkuu wa Idara ya Afrika katika Shirika la Maendeleo la Uswisi Nicolas Randin alisema wanaridhishwa na hatua zinazochukuliwa na serikali kupitia TASAF katika kupunguza umasikini nchini.
Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Ruvu Darajani Asia Mayange alisema utekelezaji wa mpango wa TASAF unaohusisha miradi ya ajira za muda pamoja na uwezeshwaji kwa walengwa umesaidia kuongeza mzunguko wa fedha pamoja na kuinua hali za maisha kwa walengwa.
“Pia walengwa wamekuwa na uwezo wa kushiriki kwenye miradi ya maendeleo ambayo inanufaisha wanakijiji wote kwa ujumla, kwa kweli tunajivunia uwepo wa TASAF hapa kwetu,” aliongeza.
Utelekezwaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini umewezesha walengwa wa TASAF katika kijiji cha Ruvu Darajani kujikita katika shughuli mbalimbali za ujasiriamali ambazo zinawaingizia kipato cha kumudu mahitaji muhumu.
Pia walengwa hao wameweza kujiunga katika vikundi vya kuweka na kukopa ambayo vinawasaidia katika kuongeza mitaji ya biashara zao pamoja na kujikita katika kilimo na ufugaji.