Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Kikundi cha walengwa chawekeza kwenye kilimo cha miti


Mwenyekiti wa kikundi cha Ahsante katika kijiji cha Ibumila Joyce Kilasi akionesha sehemu ya shamba la miti linalomilikiwa na wanakikundi ambao ni walengwa wa TASAF katika Mkoa wa Njombe

Walengwa wa TASAF katika kijiji cha Ibumila Halmashauri ya Wilaya ya Njombe wamefanikiwa kuwekeza kwenye shamba la miti kama sehemu ya uwekezaji utakaowawezesha kuwa na kipato endelevu.

Walengwa hao ambao wamejiunga katika kikundi cha kuweka, kukopa na kusaidiana pindi wanapokuwa na uhitaji kinachoitwa Ahsante, pia wanajishughulisha na biashara ndogondogo kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kila siku.

Mwenyekiti wa kikundi hicho Joyce Kilasi  amesema  wazo la kuanzisha mradi huo  lilianzishwa kutokana na uhitaji wa kuwa na uwekezaji wa kudumu  utakaonuifaisha kaya za walengwa.

“Kikundi chetu kina walengwa kumi na moja ambapo tumewekeza kwenye kilimo cha miti ya milingoti ambayo tutaivuna baada ya miaka saba, uwekezaji huu una tija na tunatarajia kupata faida kubwa kwa kuwa kuna soko la uhakika,” alisema.

“Kwa kuanzia, tulichanga hela kutokana na ruzuku tunayoipokea ambapo tulikodi shamba na kupanda miti, tumeivuna na kurudisha shamba kwa mwenye nalo na ndipo tukanunua la kwetu lenye miti tayari kwa gharama ya shilingi milioni 1.1,” aliongeza.

Kikundi hichio pia kimenunua shamba jingine ambalo wanatarajia kupanda miti mapema mwezi wa kwanza,hatua ambayo itaongeza kiwango cha uwekezaji  wao kwa maendeleo ya  kaya zao.

Akitoa shukurani kwa Serikali pamoja na TASAF, Mwenyekiti wa Kikundi ch Ahsante, Joyce Kilasi amesema wanashukuru kwa kuwezeshwa kupitia ruzuku na hivyo kumudu gharama za maisha pamoja na kuwekeza sehemu ya fedha kwenye miradi endelevu, Lengo lao ni kuboresha maisha,  wanakikundi wote wamejenga nyumba bora na zilizoezekwa kwa bati, pia wanajishughulisha na kazi mbali mbali zinazowaingizia kipato hivyo kupunguza umasikini.