Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DR. JOHN POMBE MAGUFULI AZINDUA KIPINDI CHA PILI CHA AWAMU YA TATU CHA TASAF.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John Pombe Joseph Magufuli amezindua rasmi kipindi cha Pili cha utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii- TASAF katika sherehe zilizofana na kuhudhuriwa pia na Marais Wastaafu Mhe. Ali Hassan Mwinyi, Mhe. Benjamin William Mkapa, Dr. Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wengine akiwemo ,Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ,Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.

Rais Dr. John Pombe Joseph Magufuli (wa kwanza kulia) akifuatiwa na Marais Wastaafu Jakaya Mrisho Kikwete,Ali Hassan Mwinyi na Benjamin William Mkapa wakionyeshaKitabu cha Mwongozo wa Utekelezaji wa Shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wakati wa uzinduzi wa Kipinchi cha Pili Cha Awamu ya Tatu ya TASAF.

Akizundua kipindi hicho cha pili, Rais Mhe. Dr. Magufuli licha ya kupongeza mafanikio yaliyopatikana tangu kuanzishwa kwa Mfuko huo wa Maendeleo ya Jamii mwaka 1999-2002,amesisitiza umuhimu wa kutumia fursa hiyo iliyobuniwa na serikali kuwahudumia wananchi hususani wale wanaoishi katika mazingira ya umaskini uliokithiri ili hatimaye waweze kuondokana na adui huyo mkubwa wa ustawi wa wananchi.

Aidha Rais Magufuli ametumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi mbalimbali hususani , wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi wa wilaya na watendaji wa vijiji kusimamia kwakaribu miradi inayotekelezwa kwenye maeneo yao kupitiaTASAF ili iweze kukamilika kwa wakati naq kuleta tija stahiki.

‘’mojawapo ya vigezo nitakavyotumia kupima utendaji kazi wenu ni kuona namna mlivyosimamia shughuli za TASAF kwenye maeneo yenu’’ alisisitiza Rais Dr. Magufuli.

Rais Magufuli pia ametaka shughuli za TASAF zielekezwa kwenye maeneo yote nchini ili kuwawezesha wananchi wote kunufaika ka usawa na kuondoa dhana ya baadhi yao kuona kuwa wamesahaulika kwani fursa hiyo imetolewa na Serikali kwa lengo la kusaidia jitihada za kupambana na umaskini nchini.

Rais Magufuli pia aliagiza kuandaliwe utaratibu utakaowezesha Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wenye uwezo wa kufanya kazi ,kutumia uwezo walionao kufanyakazi kwenye miradi ya maendeleo kwenye eneo husika na kisha kulipwa ujira kama njia mojawapo ya kuwaongezea kipato na kuboresha maisha yao badala ya kuwapatika ruzuku bila kufanya kazi.

Katika Kipindi cha Kwanza cha awamu ya tatu ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Serikalikupitia TASAF ilifanikiwa kutekeleza Mpango huo kwa asilimia 70 ya vijiji vyote nchini ambapo asilimia 30 ya vijiji haikufikiwa hali iliyoleta manung’uniko kwa baadhi ya wananchi waliokuwa na hamu ya kunufaika na huduma za Mpango huohasa baada ya kuona manufaa wanayoyapata Wananchi ambao walipata fursa ya kujumuishwa kwenye huduma za Mpango huo.

Kwa upande wake, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd alipongeza mafanikio yaliyopatikana katika kisiwa cha Unguja na Pemba ambako TASAF imechangia kwa kiwango kikubwa kuboresha maisha ya Wananchi na kutaka mchango huo uimarishwe zaidi kwani amesema miradi inayotekelezwa na Mfuko huo imekuwa chachu katika kuwaunganisha wakazi wa visiwa hivyo .

Akimkaribisha Rais Magufuli kuzindua Kipindi cha pili cha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini, Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala Bora, Kapteini Mstaafu George Huruma Mkuchika alipongeza uamuzi wa serikali ya awamu ya tano kuruhusu kipindi hicho kutekelezwa katika mikoa yote nchini hali ambayo alisema itasaidia kuondoa malalamiko kutoka kwenye meneo ambayo hayakufikiwa katika kipindi cha kwanza.

Hafla ya uzinduzi wa Kipindi cha Pili cha Utekelezaji wa Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASAF uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam pia ulihudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali,Vyama vya Siasa na wawakilishi wa mashirika mbalimbali ya kimataifa ambayo yamekuwa yakifanyakazi kwa karibu na TASAF.

Awali akielezea Mchango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF katika kuboresha maisha ya wananchi,Mkurugenzi wa Takwimu nchi Dr. Albina Chuwa alibainisha kuwa utafiti uliofanywa na Taasisi yake unaonyesha kuwa hali ya kipato katika kaya za Walengwa wa Mpango wa kunusuru Kaya Maskini kimeboreshwa ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kabla ya kuanza utekelezaji wa Mpango huo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF,Bwana Ladislaus Mwamanga alitumia fursa hiyo kuelezea mafanikio yaliyopatikana tangu kuasisiwa kwa Mfuko huo hususani katika Nyanja za elimu, afya,maji hifadhi ya mazingira, ujenzi wa barabara hususani zinazounganisha maeneo ya vijijini, na kuhamasisha wananchi kuanzisha miradi ya kiuchumimambo ambayo amesema yamesaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha maisha ya wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya TASAF wakati wa hafla ya uzinduzi wa kipindi cha pili cha Awamu ya Tatu ya Mfuko huo.


Rais John Pombe Magufuli (aliyeketi katikati ) akiwa katika picha ya pamoja na Baadhi ya maafisa wa taasisi za kimataifa baada ya kuzindua kipindi cha pili cha awamu ya Tatu ya TASAF.


Baadhi ya watumishi wa TASAF wakifuatilia kwa makiniuzinduzi wa Kipindi cha pili cha Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dr. John Magufuli.