Habari
Walengwa TASAF wapongezwa kwa kushiriki miradi ya maendeleo

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewapongeza wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini kwa kushiriki katika shughuli za maendeleo zenye tija. Wanufaika hao wametekeleza mradi wa barabara katika mtaa wa Bonde Kati B kata ya Kigera.
Mheshimiwa Kikwete amewataka walengwa kuendelea kutumia fursa zinazotokana na TASAF kujiimarisha kiuchumi ili kuondokana na hali ya umasikini uliokithiri.
Mhe Ridhiwani yuko kwenye ziara katika Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara kwa lengo la kutembelea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Walengwa wa Mpango katika Mkoa wa Mara.
“Nawapongeza kwa namna mnavotumia fursa iliyoletwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF na kujiondolea hali ya umasikini, Serikali inaendelea kuwahudumia wananchi kupitia programu mbalimbali ambazo zina lengo la kuboresha maisha ya wananchi wenye hali duni,” alisema.
Aidha, Mhe. Ridhiwani aliwahakikishia walengwa kuwa Serikali inafanyia kazi changamoto ya kuchelewa kupata malipo ya ruzuku zao.
Katika ziara yake, Mhe. Ridhiwani pia alionana na walengwa Joseph Nyawelesa na Zena Abeid kutoka kata ya Bonde Kati B, ambao wanaendelea na ujenzi wa nyumba za kisasa.
“Nimeanza ujenzi wa nyumba naamini ujenzi ukikamilika nitaweza kuondokana na adha ya kukosa makazi bora,” alisema Bw Nyawelesa.
Kwa upande wake Bi Zena amesema ruzuku ya TASAF imemuwezesha kufanya biashara ya uchuuzi wa dagaa ambao umemfanya aweze kuanza ujenzi wa nyumba ya kisasa.
“Ujenzi huu nimeufanya kupitia ruzuku ninayoipata, nimeweza kuweka akiba kiasi na kuitumia kwenye biashara ambapo faida ninayoipata ndio imenifanya niaze taratibu ujenzi huu wa nyumba ya vyumba viwili vya kulala,” alisema.
Katika ziara hiyo, Mhe Ridhiwani aliahidi kuwaunga mkono walengwa hao kwa kuwanunulia bati ili wakamilishe ujenzi wao ndani ya muda mfupi.