Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Serikali yafanya mageuzi ya kimtazamo katika nafasi za uongozi kwa wanawake


Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya imezindua rasmi kampeni ya inspire to lead yenye lengo la kubadilisha fikra na mitazamo ya jamii kuhusu usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi.

Uzinduzi huo umefanyika jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo maofisa habari kutoka wizara mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya kiraia, ikiwemo TASAF ambayo iliwakilishwa na Afisa miradi, ufuatiliaji na tathimini, Bi. Patricia Matogo na Afisa Habari wa Taasisi hiyo Bi. Samira Kiango

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima amesema kampeni hiyo inalenga pia kuongeza hali ya kujiamini kwa wanawake na wasichana pamoja na kuwawezesha kushiriki katika masomo ya sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM).

“Hatuna budi kushirikiana kwa pamoja kwani kampeni hii si ya Wizara moja au Serikali pekee, ndiyo maana tumewaalika wadau mbalimbali ili kwa pamoja tujenge jamii yenye usawa wa kijinsia,” amesema Dk. Gwajima.