Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Uswisi yaahidi kuendeleza ushirikiano na TASAF katika kupunguza Umaskini


Serikali ya Uswisi imesisitiza nia yake ya kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia Mfuko wa Mendeleo ya Jamii TASAF, kwa lengo la kusaidia kaya zenye uhitaji mkubwa zaidi nchini.

Akizungumza mara baada ya kikao maalumu kilichofanyika jijini Dar es Salaam, Bw. Holger Tausch, Mkuu wa Ushirikiano wa Kimataifa na Naibu balozi wa Uswisi, alisema kuwa TASAF ni mpango muhimu unaoendana moja kwa moja na vipaumbele vya maendeleo vya Uswisi.

“Tumefanya kikao kizuri sana na watu kutoka TASAF. TASAF ni mpango muhimu sana kwa Tanzania. Hata kama utapunguzwa kidogo katika siku zijazo, bado utalenga kusaidia masikini na masikini zaidi nchini jambo ambalo ndilo hasa Uswisi inapenda kuliunga mkono. Ndiyo maana tutaendelea kuunga mkono TASAF siku zijazo,” alisema Bw. Tausch.

Kikao hicho kilijadili mafanikio ya awamu ya pili ya mpango huo, ambayo imetekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Uswisi. Pande zote mbili zimekubaliana kuendeleza ushirikiano huu katika awamu ijayo inayotarajiwa kuanza mwezi Novemba 2025.


Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shedrack Mziray, alieleza kufurahishwa kwake na usaidizi wa muda mrefu kutoka Uswisi, na kusisitiza kuwa mpango huo umeleta mabadiliko makubwa kwa kaya nyingi maskini.

“Tumekuja hapa kukutana na Ubalozi wa Uswisi ambao wamekuwa washirika wakubwa katika utekelezaji wa awamu ya pili ya TASAF. Tumekubaliana kuwa programu hii imeleta manufaa makubwa sana, na tumefarijika kuona kuwa wanatambua kazi kubwa inayofanyika kati yao na serikali. Wametuhakikishia kuwa wataendelea kushirikiana nasi katika awamu mpya itakayoanza mwezi Novemba,” alisema Bw. Mziray.

Ushirikiano unaoendelea kati ya TASAF na Serikali ya Uswisi unaonesha dhamira ya pamoja ya kupambana na umaskini kupitia mikakati endelevu na yenye matokeo kwa walengwa.