Habari
TASAF bado inahitajika kwa Maendeleo na Ustawi wa Jamii

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene akizungumza na watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF (hawapo pichani) alipotembelea Mfuko huo
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Shedrack Mziray akitoa taarifa fupi kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene alipotembelea Ofisi za TASAF
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene (aliyeketi katikati) na Naibu wake Mhe. Ridhiwani Kikwete (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya Menejimenti ya TASAF
Mchango wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF kwa ustawi na maendeleo ya wananchi ni mkubwa na bado unahitajika. Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF. Mhe. Simbachawene, ambaye aliambatana na Naibu wake, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema mchango wa taasisi hiyo ni mkubwa kwa kuwa bila Mfuko huo hali ya umaskini ingekuwa mbaya zaidi ya ilivyo sasa.
Mhe. Simbachawene amesema takwimu zinazotokana na tafiti za utendaji wa TASAF zinaonesha kuwa hali ya umaskini ulivyo sasa ungekuwa juu kwa asilimia mbili zaidi bila uwepo wa TASAF katika kukuza uchumi wa walengwa wa Mpango huu.
Kutokana na miradi inayotekelezwa na TASAF ikiwemo uhawilishaji fedha, ajira za muda na ukuzaji wa uchumi wa kaya, hali ya umaskini wa chakula imeshuka wakati uandikishwaji watoto shuleni umeongezeka.
Akizungumza awali, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete alipongeza TASAF na kusema kuwa inagusa maisha ya wananchi wa kawaida na kuitaka kujikita zaidi katika malengo hayo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Shedrack Mziray alishukuru Serikali na Wadau wa Maendeleo kwa kuongeza fedha kiasi cha dola za kimarekani 200 milioni ili Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa uendelee na utekelezaji hadi September 2025. Awali kipindi cha Pili cha awamu ya tatu ya TASAF kilipangwa kukamilika Septemba, 2023.