Habari
Wanafunzi kutoka kaya za walengwa wa TASAF kupata Mikopo ya Elimu ya Juu

Wanafunzi wanaotoka kaya za walengwa wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ambao wamedahiliwa na kuwa na sifa za kuingia katika vyuo vinavyotoa elimu ya juu watanufaika na mkopo wa elimu ya juu kwa asilimia 100. Hatua hiyo inakuja baada ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kuingia makubaliano na TASAF yatakayowezesha wanufaika kutoka kaya za walengwa wa TASAF wenye sifa za kujiunga na elimu ya juu ambao wamedahiliwa na kutuma maombi kupata mikopo hiyo
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo Bw. Abdul-Razaq Badru wakitia saini mikataba ya makubaliano ya kufanya kazi pamoja.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Ladislaus Mwamanga alisema mifumo wa TEHAMA ya taasisi hizi mbili itakapounganishwa itaharakisha kubadilishana taarifa na kutoa huduma kwa walengwa. Akizungumza katika hafla ya utiaji saini makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya TASAF Dkt. Moses Kusiluka alisema asasi hizo mbili zitaunganisha mifumo yao ya TEHAMA ili kuwezesha kubadilishana taarifa za walengwa ili kuepusha udanganyifu kutoka kwa waombaji wasio waaminifu. Alisema kanzidata ya TASAF ina majina ya wanafunzi 782 waliotoka kaya wa walengwa wa TASAF ambao sasa wanapata mkopo wa elimu ya juu kwa asilimia 100 na kwa mwaka ujao inatarajiwa kuwa na wanufaika wengi zaidi.
Mwenyekiti wa Bodi ya TASAF Dkt. Moses Kusiluka akizungumza wakati wa utiaji saini
Naye Mkurugenzi wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema kwa mwaka wa masomo 2022/23 kuna wanafunzi 2,300 walioko shule za Sekondari ambao wananufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa wa TASAF ambao baada ya miaka miwili wataingia elimu ya juu na hivyo kuweza kupata mikopo ya kuendelea na vyuo vya elimu ya juu kwa wale ambao watakuwa na vigezo stahiki na kukamilisha udahili. Alisema dirisha na kuomba mkopo kwa njia ya mtandao litafunguliwa Septemba 20, 2021 hadi Septemba 30, 2021 ili kuwawezesha wale ambao walikuwa hawajaomba kuomba. Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo aliitaka HESLB iandae taarifa ya utekelezaji wa ushirikiano na kuiwasilisha kwake mara mbili kwa mwaka. Aliitaka HESLB kubaini wadau wengine wa kushirikiana nao ili kuanua wigo wa kutambua wanaostahili kupata mikopo ya elimu ya juu
Sebastian Inoshi, aliyemwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini