Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

TASAF yakamilisha Ujenzi wa Nyumba za Walimu, yasisitiza utunzaji


Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF umekamilisha ujenzi wa majengo mawili ya nyumba za walimu yenye mfumo wa 2 kwa 1 zilizojengwa  kwenye shule ya Sekondari Chitego katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mkoa wa Dodoma kwa gharama ya  shilingi  milioni 188.4.

Kukamilika na kukabidhiwa kwa nyumba hizo kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, kunatoa fursa ya kuanza kutumiwa na walimu wa Shule ya Sekondari Chitego ikiwa ni sehemu ya juhudu za TASAF katika kusaidia uboreshaji wa mazingira ya kufundishia na kuboresha  upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo elimu.

Hafla ya makabidhiano ya nyumba hizo ilifanyika shuleni hapo Mgeni Rasmi akiwa ni Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia, Mheshimiwa Job Ndugai, huku TASAF ikiwakilishwa na ndugu Salim Mshana.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Ndugai aliwataka walimu kuzitunza nyumba hizo ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na wengine waweze kuzitumia.

Aliishukuru TASAF kutokana na mchango walioutoa kwenye ujenzi huo lakini pia aliwashkuru wananchi wa Kongwa kutokana na kutoa ushirikiano pindi ujenzi wa nyumba hizo unafanywa.

“Kupitia ujenzi huo, TASAF imeondoa kero ya nyumba kwa walimu wa Shule ya Sekondari Chitego baada ya kugundulika wanatembea umbali mrefu kufika shuleni hapo na kuwajengea nyumba nne za makazi ya walimu ndani ya eneo la shule hii,” alisema.

 Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Shedrack Mziray, Afisa Uwezeshaji, Ufuatiliaji na Ushauri Bw Salim Mashana alisema baada ya kusikia shule hiyo ina uhaba wa nyumba za walimu waliamua kutoa kiasi cha fedha shilingi milioni 188.4 kwa ajili ya kujenga nyumba hizo ili kuwapunguzia adha walimu ya kutembea umbali mrefu kufika shuleni hapo.

"Tunaishukuru Serikali ya Wilaya pamoja na kamati ya usimamizi kutokana na ushirikiano iliotoa kipindi chote cha ujenzi wa nyumba hizo, ushirikiano huo uendelee hata kwenye matunzo ya nyumba hizo na kufanyiwa ukarabati kila inapohitajika", alisema Mshana.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa nyumba hizo Mkuu wa Shule ya Sekondari Chitego Bw. Born Mwakalasya alieleza kufurahishwa na ujenzi huo kwani awali walikuwa wakitembea umbali mrefu kufika shuleni hapo kitendo kilichowafanya kukosa muda wa kutosha wa kuwasaidia wanafunzi hasa nyakati za mvua.

“Kukabidhiwa kwa nyumba hizi kumeondoa changamoto ya kutembea umbali mrefu na pia imeondoa adha ya uchelewaji wa kufika shuleni na kutufanya sasa kuwahi vipindi mbalimbali vya masomo asubuhi kama vilivyopangwa”, alisema Mkuu wa Shule; akiongeza,

"Tunaishukuru sana Serikali kupitia TASAF kwa kutekeleza ujenzi wa mradi wa nyumba za shule hiyo, tunaomba waendelee kutoa msaada huo ili kusaidia ujenzi wa nyumba za walimu waliobaki".

Mkuu wa Shule huyo alisema kuwa wanaishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu na kupelekea shule mbalimbali kufanyiwa maboresho hususani kwenye ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo.