Habari
TASAF kupokea msaada wa zaidi ya Sh. bilioni 50 kutoka Uswisi, Ireland
Serikali ya Tanzania imepewa msaada wa shilingi bilioni 50.13 kwa ajili ya kufadhili Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kipindi cha Pili PSSN II unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF.
Kati ya fedha hizo, zaidi ya Sshilingi 45.09 bilioni zimetolewa na Serikali ya Uswisi na zaidi ya shilingi 5 bilioni zikitoka Serikali ya Ireland.
Akizungumza wakati wa kusainiwa kwa mikataba hiyo miwili, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Natu Mwamba amesema utekelezaji wa PSSN II unaogharimu zaidi ya shilingi 2.2 trilioni unaendana na dira ya Tanzania ya Mandeleo ya mwaka 2025.
PSSN II ilizinduliwa Februari 2020 baada ya kufungwa kwa awamu ya kwanza ya mpango wa kunusuru kaya masikini (PSSN I) Desemba 2019.
Lengo la programu hiyo ni kunguza umaskini na kuboresha rasilimali watu, kuboresha upatikanaji wa fursa za vipato na huduma za kijamii na kiuchumi kwa walengwa ambao ni kaya maskini.
"Pia programu hii imelenga kuboresha maendeleo ya watoto wao kupitia kupata fursa ya kujihusisha katika shughuli bora za kujipatia kipato, kuongezeka kwa mahudhurio ya wato wao shuleni na kwenye vituo vya afya, kuongeza uwezo wao wa kumiliki rasilimali na huduma kwa kaya maskini," amesema Dk Mwamba.
Akizungungumza katika hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Shedrack Mziray aliwashukuru washirika wa maendeleo kwa kuendelea kufadhili utekelezaji wa afua mbalimbali za kunusuru kaya masikini, huku akiahidi usimamizi thabiti wa fedha zinazotolewa kwa ajili ya mpango.
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dk Natu Mwamba (kushoto) na Balozi wa Ireland nchini Mary O’neil Tanzania wakionesha hati za makubaliano ya msaada wa Dola za Marekani milioni 2.3 kwa ajili ya utekelezwaji wa Mpango wa kunusuru Kaya Masikini Kipindi cha Pili (PSSN II)
Amesema si kwa mara ya kwanza Serikali hizo kutoa msaada kwa ajili ya utekelezaji programu hizo kwani Serikali ya Uswiss imeshatoa Sh42.5 bilioni na Ireland zaidi ya Sh10.02 bilioni.
"Fedha ambazo tumeshapata na tulizopata sasa zimetuwezesha sasa kufikia walengwa milioni 1.3 nchi nzima ambao wanahudumiwa kupitia maeneo mbalimbali ikiwemo utoaji wa ruzuku, kutoa ajira za mida kwa walengwa zaidi ya 660,000," amesema Mziray
Aidha Mziray alitumia nafasi hiyo pia kueleza kuwa walengwa wanaofanya vizuri ili waweze kufanya malengo mbalimbali wamekuwa wakipewa ruzuku maalumu.
Kwa upande wake Balozi wa Uswiss nchini Tanzania, Didier Chassot amesema kwa kushirikiana na wadau wa maendelo wengine wataendelea kusaidia kuondoa umasikini uliokithiri nchini kupitia mpango wa PSSN II
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Shedrack Mziray akizungumza wakati wa halfa ya kutia saini hati za makubaliano ya msaada wa zaidi ya Sh bilioni 50 kati ya Tanzania na nchi za Uswiss na Ireland kwa ajili ya Kipindi cha Pili cha utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini
Alisema, Uswiss na Tanzania zimekua na ushirikiano mzuri kwa zaidi ya miaka 40 na kwamba kutolewa kwa msaada huo kutaimarisha zaid mashirikiano pamoja na hali za maisha katika kaya za walengwa.
“Tangu mwaka 2020, Uswiss imekua ikisaidia utelekezaji wa mpango wa kunusuru kaya masikini kwa kutoa jumla ya dola za Marekani milioni 17.2, na leo katika halfa hii tunatarajia kutoa jumla ya dola za Marekani 17,895,000,” alisema
Mary O’neil ambaye ni Balozi wa Ireland nchini Tanzania amesema tangu mwaka 2021 serikali ya nchi yake imeelezeka zaidi ya Sh.16 bilioni kwa ajili ya kusaidia kaya maskini na zenye uhitaji nchi Tanzania huku akieleza kuwa kile kilichofanyika ni muendelezo wa ushirikiano mzuri baina ya nchi hizi mbili.
Katibu Mkuu Ikulu Mululi Mahendeka (katikati) na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dk Natu Mwamba (wa pili kushoto) wakiwa ooamoja na washirika wa maendeleo pamoja na wakurugenzi wa TASAF. Wa pili upande wa kulia kwa waliokaa ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Shedrack Mziray, na wapili kulia kwa waliosimama ni Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TASAF Godwin Mkisi
Amesema dira hiyo inatoa mwelekeo wa juhudi za kuleta mendeleo ya nchi kiuchumi na kijamii hadi kufikia mwaka 2025. "Tunatumaini kufikia malengo yaliyokusudiwa na PSSN II itakapofika mwisho wake mwezi Septemba 2025, kwa kuzingatia kwamba tumeshuhudia mafanikio kama kuwezesha kaya maskini kupata huduma za kijamii na kiuchumi," amesema Dkt. Mwamba.