Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

TASAF kuzifikia kaya zote maskini nchini


Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF utazifikia kaya zote nchini katika Vijiji, Mitaa na Shehia zote Tanzania Bara na Unguja na Pemba wakati wa utekelezaji wa Kipindi cha Pili cha Mpango wa Kunusuru Kaya za walengwa wa TASAF kilichoanza 2020 mpaka 2023.Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bwana Ladislaus Mwamanga alipokuwa akitoa mada wakati wa Semina ya kujenga uelewa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa iliyofanyika Jijini Dodoma tarehe 9 Septemba 2021. Mwamanga alieleza kwamba zoezi la kutambua walengwa wapya ambao hawakufikiwa kwenye Kipindi cha Kwanza limeshakamilika na kazi inayoendelea sasa ni kuchakata takwimu zilizokusanywa wakati wa kuwatambua walengwa hao wakati wa utambuzi.

Awali, akitoaneno la utangulizi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa alisema Serikali imetenga fedha za kutosha kuzifikia kaya zote zenye uhitaji na kuwataka wajumbe wa kamati hiyo kufanya ufuatiliaji ili kaya zote zinazostahili kupata ruzuku zinanufaika. “Toeni taarifa kama kuna kaya zilizosahaulika ili watendaji wetu wazifikie na kukamilisha taratibu za uandikishaji na Serikali itahakikisha kila Mtanzania anayestahili kunufaika na Mpango huu, anapata ruzuku,” Aliwasisitiza Mhe. Mchengerwa

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) alipongeza juhudi za Serikali katika kupunguza umaskini kwa wananchi wake na kutoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha hizo na kwamba uamuzi huo unaonesha nia ya dhati ya Serikali kuzikwamua kaya zinazoishi katika mazingira duni

 

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole akifungua semina kuhusu Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa wa TASAF.

          Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole akifungua semina kuhusu Mpango wa Kunusuru 

 Kaya za Walengwa wa TASAF. 

Akiwasilisha mada kuhusu Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa wa TASAF kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga alisema, idadi ya kaya za walengwa katika utekelezaji wa Mpango wa TASAF, Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu inatarajiwa kufikia milioni moja laki nne na nusu, hivyo wanufaika kwenye kaya hizo watakuwa zaidi ya watu milioni 10.

Bw. Mwamanga amesema, zoezi la utambuzi wa kaya za walengwa ulifanywa kwa kushirikisha jamii na viongozi katika maeneo husika ambao walikula viapo vya uadilifu na kuahidi kwamba zoezi litafanyika kwa weledi bila upendeleo wala udanganyifu

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw Ladislaus Mwamanga akiwasilisha mada kuhusu Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa wa TASAF

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw Ladislaus Mwamanga akiwasilisha mada kuhusu Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa wa TASAF

 

Wakati wa majumuisho ya semina hiyo wajumbe waliochangia mada baada ya semina hiyo waliahidi kuwa mabalozi wazuri wa kuhamasisha wananchi kufanya shughuli za kujiongezea kipato na kuwasisitiza walengwa wa TASAF kutumia vyema ruzuku wanayopata na kuanzisha miradi yenye tija ambayo itawapatia kipato na kujiimarisha kiuchumi. 

Semina hiyo ilihudhuriwa pia na Katibu Mkuu Ikulu Ndg. Moses Kusiluka na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejiment ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi.