Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

TASAF itangazwe kama mradi wa kimkakati – Ndejembi


Naibu  Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi  amewataka  Waratibu wa TASAF katika maeneo yao kutumia vyombo vya habari kuitangaza TASAF kama moja ya miradi ya kimkakati kwa kuwa mradi huu unatoa fedha nyingi zinazowafikia wananchi moja kwa moja. Rai hiyo imetolewa na Ndejembi alipokuwa ziarani mkoani Songwe.

Akizungumza na maofisa hao mjini Vwawa Mhe. Ndejembi alisema mradi wa TASAF una bajeti ya shilingi 2.2 trilioni lakini pia kupitia mkopo kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) TASAF imetengewa fedha ambazo zitatumika kwa walengwa. 

“Fedha za mkopo wa IMF ni Sh 1.3 trilioni na zimekuwa na matokeo makubwa sana kwa wananchi,  TASAF peke yake ina jumla ya Sh2.2 trilioni, lakini hatusikii TASAF ikizungumziwa sana kama miradi mingine ya kimkakati kama vile SGR na Stiegler’s Gorge (Mradi wa Kufua Umeme wa Mwalimu Nyerere – JNHHP),” alisema.

Mhe. Ndejembi alitoa changamoto kwa watendaji wa TASAF ngazi ya Maeneo ya Utekelezaji (PAA) kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake kuelimisha umma manufaa makubwa ya TASAF.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Oscar Maduhu (aliyesimama kushoto) akifafanua wakati Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ( wa tatu kutoka kushoto) alipokuwa akizungumza na watendaji wa TASAF wa Maeneo ya Utekelezaji ya Mkoa wa Songwe, mjini Vwawa Januari 20, 2022.

Aliwataka kufanya kazi muda wote na sio wakati wa malipo tu, ili kuweza kufikisha elimu kwa wananchi wa kada zote na kupunguza malalamiko yanayotokana na kutoelewa vema mchakato wa kupata walengwa wa TASAF pamoja na vigezo vyake.

Katika ziara yake katika mikoa ya Rukwa na Songwe,  Mhe. Ndejembi , amesisitiza kaya za walengwa wa TASAF kujitegemea na kuunganishwa katika vikundi ili kupata mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri.

“Ikiwa walengwa hawana maslahi ya pamoja yanayowawezesha kuunda vikundi, watengenezeeni mazingira ya kuwa na maslahi ya pamoja na kubuni miradi itakayowaunganisha katika vikundi,” alisema na kutoa mfano wa Kongwa ambapo akiwa Mkuu wa Wilaya hiyo aliunganisha vikundi vilivyokuwa na biashara tofauti na kuwawezesha kuanzisha kiwanda cha kusindika maziwa.