Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Bilioni 25.6 zatumika kutekeleza miradi ya TASAF mkoa wa Njombe


Mratibu wa TASAF Mkoa wa Njombe Mussa Selemani akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango  wakati wa ziara ya wahariri wa vyombo vya habari

Jumla ya miradi 384 yenye thamani ya shilingi bilioni 25.6 imetekelezwa mkoani Njombe na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kupitia afua mbalimbali za Mpango wa kupunguza umasikini wa kipato katika kaya.

Mratibu wa TASAF Mkoa wa Njombe Mussa Selemani alisema mpango umetekeleza miradi ya ajira za muda 113, uboreshaji wa miundombinu 191 pamoja na miradi 80 ya kuongeza kipato.

“Utekelezaji wa miradi hii umesaidia kuboresha hali ya maisha kwa kaya za walengwa pamoja na kuchagiza maendeleo katika mitaa na vijiji husika katika halmashauri za Mkoa wa Njombe,” alisema wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TASAF kwenye ziara ya wahariri wa vyombo vya habari.

Katika utekelezaji wa miradi hiyo, shilingi bilioni 19.27 zilitumika kwenye miradi ya miundombinu, wakati miradi ya ajira za muda ikigharimu shilingi bilioni 7.38 na shilingi bilioni 1.89 zilitumika kwenye miradi ya kuongeza kipato cha kaya.

Alisema miradi iliyotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa, shule, nyumba za walimu, madaraja, majengo ya kutolea huduma za afya, nyumba za watumishi, upandaji wa miti ya matunda na miradi ya maji.

Moja ya miradi  iliyotekelezwa na TASAF Katika mkoa wa Njombe, pichani ni Jengo la Mama na Mtoto lililojengwa kwa gharama ya shilingi million 160 katika hospitali ya Kibena Halmashauri ya Njombe Mji Mkoa wa Njombe kwa lengo la upatikanaji wa huduma kwa wananchi

Kwa upande wa uhawilishaji fedha, jumla ya shilingi bilioni 29 zimehawilishwa kwa kaya za walengwa 25,855 tangu mwaka 2015.

Fedha hizi pia zimesidia kuongeza idadi ya watoto wanaondikishwa shule pamoja na mahudhurio ya kliniki. Hii inatokana na utolewaji wa ruzuku ya masharti.

“Idadi ya wanafunzi walioandikishwa darasa la kwanza mwaka 2023 ilikuwa 24,247 ukilinganisha na 23,116 walioandikishwa mwaka 2015,” alisema.