Habari
TASAF yakamilisha ujenzi wa kituo cha Afya Zanzibar kwa Sh. milioni 360.8

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah amezindua Kituo cha Afya katika Shehia ya Uzi Mkoa wa Kusini Unguja kilichojengwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Kukamilika kwa kituo hicho kilichogharimu jumla ya shilingi milioni 360.8, kutarahisha upatikanaji wa huduma biora za afya kwa wakazi zaidi ya 3,800 wa Shehia za Uzi na Ng’ambwa ambao hapo awali walikuwa wakizipata kwa kusafiri umbali mrefu na kulazimika kutumia gharama kubwa.
Uzinduzi wa kituo cha afya Uzi ambacho kilianza kujengwa mwezi wa tisa mwaka 2022, ni sehemu ya shamrashamra za kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele chake ni tarehe 12 Januari 2024.
Akizungumza mara baada ya kuzindua kituo hicho, Mhe Abdullah ameipongeza TASAF kwa kujenga miundombinu hiyo muhimu ya afya kwa viwango stahiki.
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdullah akipanda mti katika uzinduzi kituo cha Afya Uzi, Mkoa wa Kusini Unguja kilichojengwa na TASAF kwa gharama ya Shilingi milioni 360.8.
“TASAF wamefanya kazi nzuri ya kujenga kituo hiki cha afya, sasa ni jukumu letu kikitunza ili kudumu kwa muda mrefu kwa ajili ya upatikanaji rahisi wa huduma za afya,” alisema.
Waziri wa Afya wa Zanzibar Mhe Nassor Mazrui na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Hamza Hassan Juma walisema kukamilika kwa kituo hicho utaongeza idadi ya watu wanaopata huduma katika shehia hizo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Shedrack Mziray aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano mkubwa inaoutoa katika kufanikisha utekelezaji wa shughuli za Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini visiwani hapo.