Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

TASAF yaboresha upatikanaji wa huduma za kijamii Utiga


Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Mkoa wa Njombe umewezesha kujengwa kwa  miundombinu  ya  afya, elimu na maji katika  kijiji cha Utiga, Halmashauri ya Wanging’ombe kwa thamani ya jumla ya shilingi milioni 391.4 kwa miradi yote.

Katika kijiji hicho, TASAF imejenga zahanati, nyumba ya watumishi, vyumba vya madarasa, nyumba ya walimu, matundu ya choo pamoja na mradi kisima cha maji ambayo imelenga kurahishisha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi

Wakizungumza  wakati wa ziara ya  wahariri wa vyombo vya habari,wananchi na walengwa wa TASAF katika kijiji hicho wamesema utekelezaji wa miradi hiyo umewapunguzia gharama za maisha kwani hapo awali, walilazimika kufuata huduma hizo katika vijiji  jirani.

“Kabla ya kujengwa kwa zahanati hii, tulikuwa tunasafiri umbali mrefu kwenda Wanging’ombe kufuata huduma za afya hivyo kuongeza gharama za maisha,” anasema  Bw, Sadiki Kisakaniki, Mwenyekiti wa Kijiji cha Utiga.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mganga mfawidhi wa Zahanati ya Utega Dkt. Peter Sumuni alisema kwa wastani wanapata wagonjwa 88 kwa mwezi ambao hapo awali walikuwa wanalazimika kusafiri kwenda mbali kufuata huduma hiyo.

“Tunaishukuru Serikali na TASAF kwa kuleta miradi hii ambayo inarahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, pia tunaishi hapa hapa katika kituo cha kazi kwani tumepata na nyumba ya watumishi,” alisema.

Nyumba ya watumishi wa Zahanati ya Utiga

Kwa upande wake, Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Utiga Athumani Kindole aliishukuru TASAF kwa kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya eliumu katika shule hiyo hatua iliyoboresha ari ya kusoma  kwa wanafunzi hao.

“Madarasa haya yamepunguza mrundikano wa wanafunzi katika madarasa yetu na sasa wanafunzi wanasoma kwa nafasi,” anasema.

Vyumba vya madarasa vilivyojengwa katika shule ya Msingi Utiga