Habari
TASAF yainua kipato kwa Walengwa, yaongeza mahudhurio Kliniki, Shule

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF, kupitia ruzuku ya msingi na ruzuku za kutimiza masharti ya elimu na afya imechochea kaya kuongezeka mapato na matumizi na mahudhurio ya shule kwa watoto kutoka kaya hizo kuongezeaka kwa zaidi ya asilimia sita.
Hayo yamesemwa Ijumaa Machi 14, 2025 na Mratibu wa Malipo ya Walengwa kwa Mtandao, Josephine Joseph alipokuwa akizungumza katika Kongamano la Wadau wa Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA-TAN), ulifanyika katika hotel ya Morena jijini Dodoma.
Kongamano hilo la siku moja limebeba dhima ya kuimarisha ushirikiano endelevu wa wadau, ili kuboresha simulizi za vyombo vya habari kuchagiza maendeleo ya Taifa.
Josephine amesema TASAF ilianza kutoa ruzuku za msingi na za masharti ya watoto kuhudhurio kliniki na shule ili kuziwezesha kaya maskini kuweza kuzifikia huduma hizo bila ya vikwazo vya kipato au kutokuwa na njia bora ya kukuza kipato.
Josephine amesema kupitia kupitia elimu itolewayo kupitia afua ya ukuzaji wa uchumi wa Kaya za Walengwa zaidi ya vikundi 68,000 vimeanzishwa nchini kote na kuwa na akiba zaidi ya Sh.bilioni 7.8 ambazo zinazunguka kwenye uchumi wa nchi ambapo kati ya hizo, walengwa wamekopeshana zaidi ya Sh bilioni 3.
Pia TASAF imeanzisha afua ya miradi ya ajira za muda kwa walengwa ambapo jamii pamoja na Walengwa wa TASAF wananufaika, hali ambayo inaongeza mchango kwenye uchumi wa nchi na jamii kwa ujumla.
Aidha, amesema pia TASAF imewezesha watoto wanaotoka Kaya maskini kupata mkopo kwa asilimia 100 jambo ambalo halikuwepo awali. Mratibu huyo alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2017 hadi 2018 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ulionesha bila uwepo wa TASAF umaskini ungeongezeka kwa asilimia 7 hadi 8.