Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

TASAF yatekeleza miradi ya maendeleo vijijini


Mbunge wa jimbo la Kilolo mkoa wa Iringa Jusin Nyamoga amesema utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF imefungua barabara nyingi ambazo zinachochea shughuli za kiuchumi kwa wananchi.

 Nyamoga ameyasema hayo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe Ridhiwani Kikwete alipotembelea halmashauri ya wilaya ya Kilolo kukagua miradi inayotekelezwa na walengwa wa TASAF.

Alisema, miradi ya barabara iliyoibuliwa na kutekelezwa na walengwa wa TASAF imefungua mawasiliano baina ya vijiji vya wilaya Kilolo.

“Licha ya kutengenezwa na walengwa wa TASAF, barabara hizi zinatumika na wananchi wote, haya ni miongoni mwa mafanikio ambayo tunajivunia kutikana na utekelezwaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini,” alisema.

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe Ridhiwani Kikwete akizungumza wakati wa ziara ya kukagua mradi wa barabara uliojengwa na walengwa wa TASAF  kijiji cha  Italula, Wilaya ya Kilolo

Akizungumza katika kijiji cha Italula, Mhe. Ridhiwani alisema shilingi bilioni 51 zimetumika katika mpango wa TASAF kwenye kutekeleza miradi ya ajira za muda, kutoa ruzuku kwa walengwa pamoja na  kuweka akiba na kukuza uchumi wa kaya.

“Dhamira kuu ni kuhakikisha wananchi wanaimarika kiuchumi na kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo kwa ajili ya kaya zao na jamii nzima kwa ujumla,” alisema.

Kuhusu utembuzi wa walengwa wapya, Mwakilishi wa KaimuMkurugenzi Mtendaji wa TASAF Oscar Maduhu alisema kaya zote za walengwa wenye sifa za kuingia kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini zitaingizwa pale utaratibu wa kuandikisha walengwa wapya utakapoanza.