Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

TASAF Yashiriki Kikao Kazi Maofisa Habari Serikalini


Waziri wa Habari, Nape Nnauye akifungua kikao kazi cha maofisa habari na mawasiliano Serikalini, kilichofanyika mjini Tanga

Maofisa Mawasiliano wa Mfuko wa Maendeleo ya  Jamii - TASAF wanashiriki kikao kazi cha Maafisa Habari na Mawasiliano wa Serikali kilichoandaliwa Idara ya Habari Maelezo na Chama cha Maofisa Habari na Mawasiliano Serikalini (TAGCO). Kikao hicho kinachofanyika mjini Tanga kuanzia Mei 9, 2022 hadi Mei 13, 2022 kitaambatana na mafunzo mbalimbali kuhusu mawasiliano ya kisasa, uongozi na uandishi wa habari za miradi.

Kikao kazi hicho kimefunguliwa Jumatatu Mei 9, 2022 na Waziri wa Habari, Nape Nnauye na kubeba ujumbe ‘Mawasiliano ya Kimkakati Nyenzo Muhimu Kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi 2022’.

Akifungua kikao hicho, Waziri Nnauye alitoa changamoto kwa maofisa mawasiliano kuwa mstari wa mbele katika kuisemea Serikali hasa pale ambapo taarifa za upotoshaji zinatolewa dhidi ya Serikali.

Maofisa habari nao walipata nafasi ya kujadili Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano ambao utaanza kutumika hivi karibuni huku maofisa habari wakiwa watekelezaji wakuu wa mkakati huo.

Aidha, Nnauye aliwataka maofisa habari  kuhakikisha kuwa tovuti za taasisi zao zina taarifa mpya huku akitoa siku 14 kuanzia May 14, mwaka huu 2022 kuhakikisha tovuti zote za Halmashauri, Wizara, Wakala na Idara za Serikali  kuwa na taarifa zinazokwenda na wakati.

Ameiagiza Idara ya Habari (MAELEZO) kuandaa utaratibu wa kufuatilia utendaji wa maofisa habari kutokana na mpango kazi unaopimika ambao utaandaliwa.

Ameiagiza TAGCO kuandaa semina mbalimbali kwa maofisa habari wa Serikali ili waweze kuielewa miradi ya kimkakati ya Serikali na kuitangaza.