Habari
TASAF ilivyonufaisha walengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida
Mnufaika wa Mpango wa TASAF Bi. Elizabeth Vicent akionesha Kondoo aliofanikiwa kuwamiliki baada ya kupokea ruzuku ya uzalishaji kupitia programu ya kukuza uchumi wa kaya.
Uhawilishaji wa Ruzuku ya Uzalishaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida umefanikisha kuinua uchumi wa kaya za walengwa zilizokuwa na kipato duni.
Kaya hizo ambazo ziliingia kwenye Mpango wa TASAF mwaka 2022, sasa zimeweza kumiliki mali mbalimbali ikiwemo mifugo, kuboresha makazi sambamba na kuwa na uwezo wa kumudu mahitaji mbalimbali ya kila siku.
Bi. Elizabeth Vicent, mkazi wa Kijiji cha Ifombou ni mmoja wa wanufaika wa TASAF ambaye ameweza kumiliki kondoo, kuku, pamoja na kuanza maandalizi ya kukarabati nyumba kwa kununua bati 10 kupitia ruzuku ya msingi pamoja na ruzuku ya uzalishaji inayotolewa kupitia programu ya kukuza uchumi wa kaya.
Mnufaika huyu ambaye ni mama wa watoto watatu, anaeleza kwamba, tangu ameandikishwa kwenye Mpango na kuanza kupokea ruzuku, amekuwa akithaminiwa kwenye jamii kutokana na kuwa na uwezo wa kuchangia mahitaji mbalimbali ya familia pamoja na kuwa na shughuli ya kufanya.
“Huwa napokea shilingi 88,000 kama ruzuku kwa kipindi cha miezi miwili, fedha hiyo imekuwa inanisaidia kwenye mahitaji mbalimbali ambapo pia nimeweza kununua bati 10 kwa ajili ya nyumba, pia nilipokea ruzuku ya uzalishaji jumla ya shilingi 350,000 ambayo nilipokea kwa awamu mbili,” alieleza.
“Awamu ya kwanza nilipokea shilingi 175,000 ambayo nilitumia kununua kondoo watatu, na baadaye nikapokea shilingi 175,000 nyingine ambayo nayo nilinunua kondoo wawili na kufanya kuwa na jumla ya kondoo 5,” alisema.
Kwa kufuata miongozo na mafundisho ya ujasiliamali aliyopewa kabla ya kupokea ruzuku hiyo, Bi. Elizabeth aliweza kufanikiwa kuongeza kondoo wanne ambao walizaliwa kutokana na aliowanunua, pia amekuwa akiuza baadhi ya kuku wake ili kupata fedha za mahitaji madogo madogo wakati anasubiri fedha za ruzuku.
“Naishukuru Serikali na TASAF kwa kuleta Mpango huu wa kutusaidia, na sasa nimeweza kuwa na mali na pia nachangia kwenye kipato cha kaya kwa kusaidia manunuzi ya mahitaji muhimu,” alisema.
Kwa upande wao, Bi. Mwanahamis Mugwu na Bi. Cecilia Samwa ambao pia ni wanufaika wa Mpango wa TASAF wamesema kupitia Mpango huu wameweza kujiunga kwenye vikundi vya kuweka akiba na kukopa hivyo kujiongezea uwezo wa kuwa na fedha ya matumizi na uwekezaji.