Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Ikulu

Mfuko wa Maendeleo ya Jamii

Habari

Vikundi vya TASAF Dar vyaalikwa Zanzibar


VIKUNDI vya uzalishaji mali vinavyoundwa na walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa unaotekelezwa na TASAF vimealikwa kwenda Zanzibar ili kubadilishana uzoefu na vikundi vya jinsi hiyo.

Mwaliko huo umetolewa Februari 4, 2022 na Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Ali Suleiman Amer wakati kamati hiyo ilipotembelea miradi ya vikundi vya TASAF vilivyo Minazimirefu jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo ilikuwa katika ziara ya siku mbili jijini Dar es Salaam kutembelea miradi ya TASAF ambapo ilipata fursa ya kutembelea vikundi vinavyojihusisha na uzalishaji mali pamoja na ufyatuaji matofali ya sakafu (pavers) katika ajira za muda zinazotolewa kwa walengwa wa TASAF katika eneo la  Minazimirefu Dar es Salaam.

Katika eneo hilo kuna vikundi 10 ambavyo vimeungana katika ajira za muda kufyatua matofali na pia kuzalisha bidhaa mbalimbali pamoja na kukopeshana fedha.

 

Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa katika eneo la Minazimirefu jijini Dar es Salaam wakiwaonesha wajumbe wa Kamati ya Bajeti ya Baraza la Wawakilishi bidhaa wanazotengeneza

Amer alisema kazi zinazofanywa na vikundi hivyo ni za kupigiwa mfano na hivyo ni vema wakaenda Zanzibar ili kuwaonesha wenzao wa huko pamoja na kujifunza.

“Ninakualikeni Zanzibar mje muone wanavyofanya wenzenu na pia kuwapa uzoefu wenu…pia vikundi vya huko vitakuja huku siku si nyingi,” alisema.

Naye mjumbe mwingine wa kamati hiyo, Omar Fakih Hamad alisema TASAF ni kielelezo cha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa jinsi inavyonufaisha pande zote mbili za Muungano bila ubaguzi