Habari
Wahariri wa Vyombo vya Habari Tanzania Watembelea Miradi ya Miundombinu Njombe

Mwonekano wa madarasa yakiwa na samani zake katika shule ya Umonga
Wahariri wa Vyombo vya Habari nchini Tanzania wako katika ziara ya kutembelea Miradi ya Miundombinu inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Mkoani Njombe kwa siku tatu kuanzia 19 – 21 Desemba 2023 ambako watatembelea miradi katika Halmashauri za Mji wa Njombe, Halmashauri ya Wilaya ya Wang’ing’ombe na Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.
Katika siku ya kwanza, Wahariri hao walitembelea ujenzi Shule ya Msingi Umago inayojengwa na TASAF kupitia Miradi ya Miundombinu. Miundombinu inayojengwa katika shule hiyo ni Ujenzi wa madarasa na samani zake, Ujenzi wa Matundu ya vyoo, Ujenzi wa Uzio na Ujenzi wa Bwalo la chakula. Kwa mujibu wa Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Wilaya Njombe Mji Bi. Mariam Yohana Monjesa miradi hii yote inagharimu kiasi cha 277.1 milioni.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Umago, Bi. Adelaida Joseph Sambala amekiri kwamba shule hiyo imepunguza msongamano kwenye Shule Mama ya Msingi ya Uwemba, imepunguza utoro wa wanafunzi kwani kwa muonekano wake inawavutia wanafunzi kuhudhuria masomo na pia imeongeza ufaulu kwani katika matokeo ya darasa la Saba yaliyotangazwa hivi karibuni ni wanafunzi 37 kati ya wanafunzi 39 waliofanya mtihani huo wamefaulu.
Vyoo vya wanafunzi katika Shule ya Msingi Umago
Bwalo la Chakula kwa wanafunzi katika Shule ya Msingi Umago