Habari
Walengwa TASAF Hupatikana kwa Uwazi - Ridhiwani Kikwete

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema mchakato wa kuwapata walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) hupatikana kupitia mkutano wa wananchi wa eneo husika na mchakato hufanyika kwa uwazi pasipo na upendeleo. Mhe. Ridhiwani ameyasema hayo mbele ya Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria katika kikao cha kupokea taarifa ya utendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii kwa kipindi cha Mwezi Machi hadi Juni 2023. Alitoa ufafanuzi huo wakati akijibu hoja za wajumbe wa kamati hiyo Mhe. Abdullah Ali Mwinyi, Mhe Agnesta Lambert na Mhe. Tumaini Magessa ambao waliuliza kuhusuana na vigezo vya kuwapata walengwa pamoja na miradi mbalimbali inayotekelezwa na TASAF.
Alisema kuna utaratibu mahususi ambao unatumika katika kuwapata walengwa na wanufaika, unaanzia katika ngazi ya kijiji na mtaa, ambapo Mwenyekiti wa kijiji au mtaa huitisha kikao cha wananchi ambao ndio hupendekeza vigezo vya kaya maskini na baadae majina ya watu wenye hali duni kiuchumi ili waingie kwenye mpango. “Na utaratibu wa kuwapata walengwa huwa ni wa uwazi na shirikishi kwa watu wote, na wale ambao majina yao yamependekezwa ili waingie kwenye mpango na wale wanaotolewa kwa kutokukidhi vigezo vilivyowekwa, huwa wanapewa fursa ya kukata rufaa pale ambapo wanakuwa hawajaridhika na hatua zilizochukuliwa”, alisema Naibu waziri.
Pia, Mhe. Ridhiwani alisema wanufaika wa TASAF wanapiga hatua kila siku, akisema hadi sasa wapo walengwa wengi waliofanya vizuri kupitia mapango huu. Aliongeza kuwa hadi sasa kuna kaya 78,895 ambazo zimekidhi vigezo vya kutoka katika mpango wa TASAF, lakini wengi wao hawapo tayari kutolewa kwa hofu kuwa hawataweza kujitegemea wakiwa nje ya Mpango.
“Changamoto iliyopo ni kwamba watu wanaweza kujitokeza mbele ya hadhara kuelezea mafanikio, lakini wakiambiwa watoke nje ya mfumo ili kuwapisha wengine, hawakubali. Hili lipo maeneo mengi, tunaendelea kutoa elimu ya ujasiriamali waweze kujitegemea”, alisema Naibu Waziri. Hata hivyo, Mhe. Kikwete alisema hivi sasa Serikali inafanya tathimini ya hali za walengwa katika Maeneo 72 ya Utekelezaji.
Akizungumzia kuhusu Miradi ya Jamii, Mhe. Ridhiwani alisema miradi hiyo hubuniwa na wananchi wa eneo husika kulingana na changamoto wanayokutana nayo na kwamba utekelezwaji wake hutegemea nguvu kazi kutoka katika kaya za walengwa ambao hulipwa ujira kwa kazi hiyo. “Hii ni miradi ambayo hutumika kuzalisha ajira za muda kwa walengwa, na miradi hii hubuniwa na wananchi wa eneo husika, pale inapooneka kuna changamoto katika utelekezwaji wake, basi walengwa huruhusiwa kubadili aina ya mradi”, alisema wakati anajibu swali la Mhe. Tumaini Magessa mbuge wa jimbo la Busanda aliyetaka kujua kwa nini walengwa hufanyishwa kazi.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene alisema Serikali imekuwa ikichukua hatua za kuwaondoa kwenye mpango wanufaika wote walioingizwa kwenye mpango pasipo kukidhi sifa zilizowekwa. “Serikali imekuwa ikitoa maelekezo ya mara kwa mara ikisisitiza wanaostahili ni walengwa na kuondolewa walioingizwa pasipokuwa na sifa. Kigezo chetu ni kuchukua wananchi wenye hali ya chini ili kuwasaidia, changamoto inakuja kwenye namna ya kuwapata, lakini tunaendelea kuboresha eneo hili”, alisema Mhe. Simbachawene.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama aliipongeza Serikali na TASAF kwa kazi nzuri inayofanyika ya kuratibu na kuendelea na miradi mbalimbali ya kunusuru kaya masikini. Mhe. Dkt Mhagama alishauri TASAF kuhakikisha miradi yote ya jamii inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini inakuwa na ubora ili idumu kwa muda mrefu na kuangalia uwezekano wa kuwafanya wanufailka wa miradi hii wawe sehemu ya umiliki baada ya kukamilika kwake. “Tumeona shughuli mbalimbali ambazo zinafanyika kupitia TASAF katika kuinua na kuimarisha vipato vya kaya maskini, juhudi hizi ni nzuri na tunapendekeza kuendelea na maboresho mbalimbali katika maeneo muhimu ili kuleta tija zaidi”, alisema Mhe. Mhagama.