Habari
Walengwa TASAF wakaribishwa sokoni Kariakoo

Walengwa wa TASAF (kulia) wakizungumza na wateja waliotembelea banda la TASAF
Wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa wanaoshiriki Maonesho ya Kilimo ya Nanenane wamekaribishwa kuuza bidhaa zao za kilimo katika Soko la Kimataifa la Kariakoo, jijini Dar es Salaam.
Wanufaika hao ambao wanajihusisha na kilimo na ufugaji kutoka Mkoani Mbeya wanashiriki katika Maonesho ya Nanenane jijini Mbeya.
Akitembelea banda la TASAF, Kaimu Meneja Mkuu wa Shirika la Masoko Kariakoo, Sixbert Kaijage alisema bidhaa zinazozalishwa na walengwa wa TASAF zina ubora wa kutosha kuuzwa katika soko hilo.
“Nawakaribisheni kuuza bidhaa hizi Kariakoo, ifikapo mwakani ujenzi upya wa soko utakuwa umekamilika na mnaweza kuja kuniona mkapata eneo maalum la kuuza bidhaa zenu,” alisema Kaijage alipokuwa akizungumza na wanufaika hao wa TASAF jijini Mbeya.
Walengwa wanaoonesha bidhaa zao ni Enos Ngabo anayelima mbogamboga na viungo, Alon Sanga anayeshona vikapu, Msafiri Lwanga mfugaji wa ng’ombe anayeuza maziwa na Joina Sanga anayeonesha na kuuza karoti na mbogamboga kutoka shambani kwake na Sarah Mwandima anayeonesha na kuuza vitunguu na viazi ambavyo vinaoteshwa bila kutumia mbolea na Fasness Jaton anayeonesha na kuuza kuku.
Kaimu Meneja wa Shirika la Masoko Kariakoo, Sixbert Kaijage (kushoto) akizungumza na Sarah Mwandima ambaye ni mlengwa wa TASAF katika Maonesho ya Kilimo Nane nane jijini Mbeya