Habari
Walengwa TASAF watakiwa kujitegemea

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi akizungumza na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa katika kijiji cha Kipundi, Sumbawanga
Wanufaika wa Mpango wa kusaidia Kaya za Walengwa unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF wametakiwa kutobweteka na ruzuku wanazopata na badala yake walenge kuanzisha miradi itakayowawezesha kujitegemea. Naibu Waziri, Ofisi ya Rais
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi ameyasema hayo kwa nyakati tofauti alipotembela miradi ya TASAF pamoja na walengwa wa Mpango huo katika mikoa ya Rukwa na Songwe.
“Kuna hatari kuwa sasa wanufaika wakajijengea hali ya utegemezi na iwapo ruzuku itachewa kidogo wanaanza kulalamika…kabla ya mradi walikuwa wanakula, wanavaa na kupata mahitaji yao mengine hata kama kwa shida,” alisema na kusisitiza kuwa lengo la mradi ni kuwakwamua walengwa ili baada ya muda mfupi waweze kujitegemea.
Aliwataka watendaji wa TASAF katika maeneo yao kusisitiza zaidi katika kuwaunganisha walengwa katika vikundi vya ujasiriamali na mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri ili waweze kuanzisha miradi midogo midogo ya kiuchumi.
Hata hivyo, alielezwa kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kuna vikundi wivili na Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga pia kuna vikundi viwili vinavyotokana na walengwa wa TASAF.
Alipotembelea kikundi cha akinamama cha walengwa kiitwacho Kukombolewa katika kijiji cha Lusaka Naibu Waziri alijionea shughuli za kilimo wa kikundi hicho kinachotumia ardhi ya kukodi.
Naibu wa Waziri Ndejembi aliagiza Maofisa Ugani kutembelea kikundi hicho kutoa ushauri na akaagiza uongozi wa kijiji kuwapatia ardhi walau ekari tano.
Mratibu wa TASAF Halashauri ya Kalembo, Marium Kimashi alimwelezwa Naibu Waziri kuwa katika Halmashauri yake, walengwa 2,000 kati ya 8,634 wameomba kujitoa kwenye Mpango baaya ya kuwa hali zao ya kiuchumi zimeimarika.
Pamoja na kupongeza hatua hiyo, Mhe. Ndejembi alisema anatamani ifikapo mwishini mwa mwaka 2022, walau walengwa 15,000 katika Halmashauri hiyo wawe wamejitoa katika Mpango. Akitembelea walengwa katika Kata ya Namanjele, Mhe. Ndejembi alisema Rais Samia Suluhu Hassan anawajali wananchi wanyonge ndio maana ameongeza Sh.bil. 5.5 kwenye Mpango wa TASAF ili kaya zote maskini ambazo ni walengwa wa mpango huo zinufaike.
Alisema licha ya Rais kuelekeza fedha nyingi kwenye shughuli mbalimbali za kijamii, ameona ni vema kutenga fedha zaidi kwa ajili ya utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya za Walengwa ambao kwa kiasi kikubwa unazisaidia kaya maskini kujikwamua kutoka kwenye lindi la umaskini.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Oscar Maduhu akifafanua jambo wakati Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi alipozungumza na Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa katika kijiji cha Kipundi, Sumbawanga
“Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, imefanya kila kitu kuuongezea nguvu ya kiuchumi Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF ili uweze kutekeleza vizuri Mpango wa Kuzinusuru Kaya za Walengwa nchini, hivyo ni jukumu la kila mlengwa kuitumia vizuri ruzuku anayoipata kuboresha maisha yake,” Mhe. Ndejembi alisema.
Ili kuboresha zaidi maisha ya walengwa hao, Mhe. Ndejembi amewataka walengwa kuona umuhimu wa kuunda vikundi vya ujasiriamali ambavyo vitawawezesha kupata sifa kukopeshwa na Halmashauri.
Kwa upande wake mlengwa wa TASAF, Scolastica Tinga wa Kijiji cha Kipundi, alisema TASAF imemwezesha kusomesha mtoto wake na kuboresha makazi yake kwa kuezeka kwa bati badala ya nyasi.
Baadhi ya Walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya za Walengwa katika kijiji cha Ipundi wakimzikiliza Naibu Waziri (Ofisi ya Rais) Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deogratius Ndejembi
Naye Leatitia Futakamba alisema TASAF imemwezesha kuanzisha miradi kadhaa ya ufugaji ambapo anaweza kujipatia mahitaji yake mengine na kuomba asaidiwe kuboresha mabanda ya mifugo yake.
Kufuatia ombo hilo, Mhe. Ndejembi alitoa Sh100,000, Mbunge wa Nkasi Kaskazini Aida Kenani alitoa Sh100,000 na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Oscar Maduhu alitoa Sh 100,000 kwa ajili ya kusaidia uezekaji wa mabanda ya mlengwa huyo.