Habari
Walengwa wa TASAF Waaswa Kujiandaa Kuhitimu Kwenye Mpango

Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Bwana Steven Ndaki (aliyevaa kofia) akimsikiliza Bw. Allon Sanga ambaye ni mlengwa wa TASAF katika maonesho ya Nane Nane yaliyofanyika Mkoani Mbeya
Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Bw. Steven Mashauri Ndaki amewaasa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) kujiandaa kuhitimu kwenye Mpango huo na kuendelea na maisha ya kujitegemea bila kutegemea ruzuku baada ya kuwonekana wamefanya vizuri na kuwa imara kiuchumi. Bwana Ndaki aliyasema hayo wakati alipotembelea Banda la Maonesho la TASAF katika Maonesho ya Nane Nane yanayofanyika Kitaifa katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.
“Nawapongeza kwa hatua mliyofikia. Maelezo mliyonipa yanaonyesha kwamba mnwtumia vizuri ruzuku mliyopokea kujiimarisha kiuchumi na kutoka katika hali duni ambayo Mpango ulikuwa nayo, Naamini sasa mko tayari kuanza safari ya kujitegemea bila ruzuku ya TASAF. Anzeni maandalizi ya kuondoka kwenye Mpango na kuwapisha wengine wenye uhitaji mkiwa na mitaji ya kujiendeleza” alisema Bw. Ndaki
Naye Bi. Fasinesi Jatoni ambaye ni mlengwa kutoka katika mtaa wa Imbega kata ya Iziwa Jijini Mbeya alijinasibu kwa kusema kwamba TASAF imemnusuru kutoka katika umaskini wa kukosa hata mlo mmoja kwa siku na kumfikisha mahali ambapo anachagua aina gani ya vyakula ale yeye na kaya yake maana anavyo vingi mno.
“TASAF imeniheshimisha sana kiasi cha kunileta kwenye maonesho haya nikiwa na kuku chotara 17 ambapo kuku mmoja mdogo na tetea ninamuuza kwa shilingi 25,000 na hii imenipa hamasa sana ya kuendela na ufugaji hata baada ya kumalizika kwa maonesho haya” alisema Bi. Fasinesi.
Katika maonesho hayo, jumla ya wanufaika wa TASAF sita (06) kutoka katika vijiji na mitaa mbalimbali ya mkoa wa Mbeya wanashiriki wakiwa na bidhaa mbalimbali kama vile kuku, vikapu, mboga za majani, viazi mviringo, maziwa, vitunguu, pasheni, nyungo, ndizi na blokoli.