Habari
Walengwa wa TASAF waombwa kutengewa maeneo ya biashara

Bi. Tausi Khalfani Abdallah (aliyeshika kipaza sauti) akimweleza Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobass Katambi mambo ambayo yanafanyika kwenye vikundi wakati alipotembelea mabanda ya maonesho ya TASAF Mnazi Mmoja – Dar es Salaam.
Walengwa wa TASAF wameomba kutengewa maeneo ya kufanyia biashara ili kuuza bidhaa mbalimbali wanazotengeneza kwenye vikundi vyao vya Kuweka Akiba na Kukuza Uchumi wa Kaya. Hayo yamesemwa na mwakilishi wa walengwa wa TASAF Bi. Tausi Khalfani Abdallah wakati akimweleza Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobass Katambi kazi wanazofanya katika vikundi vyao wakati alipotembelea Mabanda ya Maonesho ya TASAF.
“Ndugu Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa niaba ya wanavikundi wenzangu wa TASAF, naomba kukujulisha kuwa kwa hatua tuliyofikishwa na TASAF, sisi siyo walengwa tena bali ni wanufaika wa TASAF. Tuomba tutafutiwe maeneo ya kufanyia biashara ya bidhaa tunazozalisha kama wanavyotengewa Wamachinga au Wajasiliamali wadogo wadogo” alisisitiza Bi. Tausi.
Naye Mheshimiwa Katambi aliwapongeza sana wanufaika wa TASAF kwa kuonesha maendeleo na mabadiliko baada ya kuwezeshwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), na kwamba maombi ya masoko na kutengewa maeneo ya biashara yatafanyiwa kazi. “Nitoe agizo kwa niaba wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Wakuu wa Mikoa wote na Wakuu wa Wilaya wote kuendelea kutenga maeneo kwa ajili ya Machinga na wanufaika wa TASAF ili wapate nafasi ya kufanya biashara zao ili waje kuwa mabilionea wa kesho” alisema Mhe. Katambi.
Pia aliwaagiza viongozi wengine wa Wizara ya Fedha na Mipango na wengine kusimamia maelekezo hayo kuhakikisha kuwa kila yanapotengwa maeneo kwa ajili ya wajasiliamali wadogo wadogo au machinga na wanufaika wa TASAF nao wanapatiwa maeneo hayo ikiwa ni moja ya njia za kuwatafutia masoko kama walivyoomba wanufaika hao.
Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Patrobass Katambi (aliyeshika kipaza sauti) akiongea na wanavikundi wa TASAF wakati alipotembelea mabanda ya maonesho ya TASAF Mnazi Mmoja – Dar es Salaam.
Akimkaribisha Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira katika mabanda ya TASAF, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Godwin Mkisi amesema kuwa katika Wiki ya Maonesho ya Huduma za Kifedha Kitaifa TASAF imewakilishwa na vikundi Nane (08) vya Kuweka Akiba na Kukuza Uchumi wa Kaya, ambapo kati ya hivyo viwili (02) vinatoka Zanzibar. “TASAF ina jumla ya vikundi zaidi ya 27,000 vya Kuweka Akiba na Kukuza Uchumi wa Kaya” alisema Bw. Mkisi.
Wakati akifunga maonesho hayo, Mgeni Rasmi, ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Emmanuel Tutuba aliwapongeza washiriki wote wa maonesho hayo, wakiwemo TASAF, kwa kuhudhuria na kutoa elimu kwa umma juu ya “Kuboresha Maisha Kupitia Elimu ya Fedha” na kwamba madarasa yaliyokuwepo yamechagiza watu kupata uelewa mpya juu ya matumizi sahihi ya fedha zao na fursa wanazoweza kuzitumia kupata fedha.
Mgeni Rasmi, ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Emmanuel Tutuba (alisimama kwenye kipaza sauti) akifungua rasmi Maonesho ya Wiki ya Huduma za Kifedha Kitaifa tarehe 14.11.2021 katika
Viwanja vya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam.
Kwa mara ya kwanza Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa Maonesho ya Wiki la Huduma za Fedha Kitaifa na kuwaleta pamoja watoa huduma wote ili kuwafanya wafahamiane na watoe elimu ya fedha kwa pamoja kwa umma. Maonesho hayo ya siku saba (07) yalianza rasmi tarehe Novemba 08, 2021 na kufungwa rasmi Novemba 14, 2021, yakiongozwa na kauli mbiu isemayo, “Boresha Maisha Kupitia Elimu ya Fedha”.